Kampeni za uchaguzi mdogo wa ubunge katika jimbo la Kalenga, Iringa vijijini zimeanza kuchukua sura mpya baada ya chama cha demokrasia na maendeleo ( CHADEMA ) kuanza kutumia helikopta ambapo kwa siku watafanya mikutano sita.....
Mwenyekiti wa chama hicho taifa, Bw. Freeman Mbowe, alisema chama hicho kitapasua anga ya jimbo hilo kupitia kauli mbiu yao ya "Anga kwa anga, Kofia na kanga sasa basi", akiongoza mashambulizi hayo ili kumpigia kampeni mgombea wao, Bi Grace Tendega....
Alisema helikopta hiyo itapita mtaa kwa mtaa, kata kwa kata, kijiji kwa kijiji, tarafa kwa tarafa.
Katika hatua nyingine, wakazi wa jimbo hilo wametahadharishwa kutoikimbilia helikopta ya CHADEMA kwa kuwa ina athari kiafya....
Katibu wa CCM mkoani Iringa, bw. Hassan Mtenga aliyaema hayo juzi wakati akimnadi mgombea wa CCM, bwa. Godfrey Mgimwa katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye kata ya Luhota, jimboni humo....
"Tunasikia CHADEMA wanataka kuleta helikopta ili kukusanya watu kwenye mikutano yao baada ya kuona wananchi hawafiki kwenye mikutano yao.Naomba nitoea tahadhari, mkiiona msiende kwani helikopta zina madhara kiafya", alisema bwa. Mtenga
Alisisiza kuwa moshi unaotoka katika injini ya helikopta una madhara kiafya na mara nyingi husababisha kansa, hivyo hakuna sababu ya kusogelea karibu...
Alisema athari za kuisogelea helikopta zinaweza zisijitokeze sasa lakini baada ya muda fulani, zitaanza kujitokeza, hivyo aliwataka wakazi wa jimbo hilo kuwa makini....
"Ushauri wangu, wakija na helikopta zao msiende, endeleeni na kazi zenu maana mkivuta moshi wa helikopta mtaathirika", alisema na kuongeza kuwa CCM inauhakika wa kushinda katika uchaguzi huo.....
Kwa upande wake bwana Mgimwa amewahakikishia wakazi wa jimbo hilo kuwa kama watampa ridhaa ya kuwa mbunge wao atamaliza tatizo la maji ambalo limedumu muda mrefu katika kijiji cha Kibena, kata ya Ifunda....
Alisema mbali ya changamoto nyingi zilizopo kijijini hapo,tatizo la maji ndio limeonekana kuwa sugu hivyo atakwenda kuzungumza na waziri wa maji, Profesa Jumanne Maghembe ili amweleze hitaji la maji kwa wanakibena...
"Ndugu zangu natambua kuwa kijiji hiki kinatatizo kubwa la maji, hivyo kama mtanipigia kura za kutosha na kuwa mbunge wenu ntahakikisha nalimaliza", alisema.
Wakati huo huo,mwenyekiti wa CHADEMA kijiji cha Wangama, bw. Fred John, ametangaza kukihama chama hicho na kujiunga CCM. Kijiji hicho ndicho alichozaliwa mgombea ubunge wa jimbo hilo kwa tiketi ya CHADEMA,Bi Tendega...
Akizungumza mbele ya viongozi wa CCM na wakazi wa eneo hilo, bw. John alisema ameamua kuhama CHADEMA kwa hiari yake kwani alikuwa anapotea....
"Niwahakikishieni wakazi wa kijiji hiki, nitarudisha wote waliokuwa CHADEMA kwani mimi ndiye niliyefanya kazi ya kuwahamasisha,sasa mwamba umevunjika", alisema
Awali, katibu wa CCM mkoani Mtwara, Shaibu Akwilombe aliwaambia wakazi wa kijiji hicho kuwa bi. Tendega hana ilani ya uchaguzi wala serikali hivyo hawezi kuleta maendeleo....
Alisema kuwa ili maendeleo yapatikane Kalenga, wananchi wanapaswa kumchagua mgombea wa CCM, Bw. Mgimwa.
"Grace ni dada yetu,ndugu yetu, rafiki yetu na jamaa yetu, lakini tusimpe nafasi ya kuwa mbunge kwa sababu CHADEMA hakina Ilani wala serikali....Mpeni kura zote Mgimwa ili aweze kuwaletea maendeleo", alisema Akwilombe

Post a Comment