0
UJUMBE mfupi wa simu ya mkononi (SMS) wa kimapenzi ambao ulitumwa kutoka simu inayomilikiwa na kiongozi wa kanisa la Ngurumo ya Upako, Nabii Geor David Kasambala kwenda kwa mke wa muumini wa kanisa hilo umesababisha ndoa kuvunjika.
 
 Mwanamke aliyetumiwa SMS na nabii huyo ni Pamela Godfrey, mke wa Wilson Lota, wote waumini wa kanisa linaloongozwa na Nabii Geor David.
 
Ndoa ya wawili hao imedumu kwa miaka minane hadi jana baada ya mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha kubariki kuvunjwa kwa ndoa hiyo. Uamuzi wa mahakama hiyo unatokana na kesi iliyofunguliwa na Lotta, akiomba ridhaa ya mahakama kupatiwa talaka, baada ya Pamela ambaye ni mke wake kuikimbia familia yake yenye watoto wanne na kuhamia kwa nabii Geor David.
 
Hakimu wa mahakama hiyo, Hawa Mguruta katika uamuzi wake alioutoa jana, alisema kutokana na ushahidi uliotolewa na mashahidi umethibitisha kuwa wanandoa hao wametengana tangu mwaka 2006 na hawawezi tena kuwa pamoja, hivyo mahakama imekubali kutoa talaka.
 
Katika hukumu aliyoisoma kwa zaidi ya saa 2:45, Mguruta, alisema ni wazi katika ushahidi umethibitika chanzo cha ndoa hiyo kuvunjika ni ujumbe mfupi wa kimapenzi kutoka kwa Nabii Geor David. Pia alisema mahakama hiyo imetilia mkazo ushahidi kutoka kwa mtoto wao mkubwa Sifaeli Wiston (15) aliyeiambia mahakama alikuwa akimwona Nabii huyo nyumbani kwao wakati baba yake anapokuwa yuko safarini.
 
Kesi hiyo ya madai namba moja ya mwaka 2012 ilifunguliwa na Lotta, dhidi ya mke wake, Pamela ambaye aliomba mahakama ivunje ndoa hiyo kutokana na mwanamke kuhamia kwa kiongozi huyo wa kidini. 
 
Hakimu Mguruta alisema mtoto huyo aliithibitishia mahakama hiyo kuwa alikuwa akimwona Nabii huyo mara kwa mara hapo nyumbani na alipomuulizia mama yake alikuwa akidai wanafanya maombi maalumu sebuleni.
 
Mtoto huyo pia alisema wakati mwingine mama yake na nabii huyo walionekana pamoja ndani ya gari la rangi ya fedha lenye pazia, ambalo walikuwa wakitumia kukaa humo ndani kwa saa kadhaa.
 
Kuhusu kugawana mali ya Kampuni ya Winston, mahakama ilisema hakuna cha kugawana kutokana na kampuni hiyo haijavunjwa na mke huyo hajachuma chochote ndani ya kampuni hiyo.
 
Hakimu pia alisema isitoshe mwanamke huyo aliondoka na kubeba baadhi ya mali zake huku akiwaacha watoto wake wote akiwemo wa miaka miwili bila kurudi nyumbani  hata kuwajulia hali.
 
"Hivyo mahakama hii inaamuru watoto pia wataendelea kukaa kwa baba yao na wewe mama utaruhusiwa kuwasalimia sababu ni haki yako ya msingi, lakini usije ukaingilia uhuru wa masomo yao," alisema hakimu Mguruta.
 
Kwa upande wa Pamela alikanusha kuwa na mahusiano ya kimapenzi na Nabii huyo huku akishindwa kudhibitisha juu ya meseji ya simu yake iliyobambwa na mume wake na kuhusu kukaa kwenye gari kwa saa kadhaa na mchungaji huyo pia hakuweza kukanusha.
 
Pamela aliomba mahakama kupewa sehemu ya mali, sababu aliondoka bila kubeba chochote baada ya kuchoshwa na mateso ya mume wake ambaye alimchukua na kumpeleka ndani ya msitu wa Olmotonyi akiwa na panga ili amuue, ila wamasai walipotokea alimwachia.
 
Awali Wiston aliiambia mahakama hiyo kuwa ni vema wakatoa talaka, kwani mke wake hajakubali kurejea nyumbani licha ya kujitahidi kumbembeleza arudi nyumbani, ila alihamia Kisongo.
 
Hivyo Lotta alisema shauri hilo ambalo lilianza kunguruma mwaka 2007, kwenye Baraza la usuluhishi wa ndoa na kushindikana kufikia uamuzi ni vema mahakama iingilie kati na kuivunja ndoa yao.
 
"Mimi sikatai nilikuwa Mkurugenzi wa huduma za kiroho kwa nabii huyu na pia nilikuwa nikiratibu mikutano yote na huduma zote za pale, ila nikashangaa kuona amenizunguka," alisema.
 
Alidai kuwa sababu za kushindikana kwa kupatikana suluhu Baraza, ni baada ya mke wake kupeleka sababu za uwongo kwamba alikuwa ananyanyaswa na kukimbia nyumba, wakati hajawahi kumpiga na yeye alimtelekezea watoto watatu wadogo hasa wa mwisho alikuwa na miaka miwili, ambao alilazimika kuwapeleka Kenya kwenye shule za bweni ili walale na kulelewa huko.
 
Pia anadai kuwa anashangazwa kusikia mke wake akidai mali wagawane, ambazo alishachukua na ndugu zake na zingine alihamishia kwa mchungaji Geor David, ambazo ni laptop yenye thamani ya dola za Kimarekani 1,300.
 
“Lakini huyu mke wangu alichukua mkopo wa dola 2000 na kumpa Mchungaji Geor David na kumkodishia gari la kampuni yake ya Winston Safari, aina ya Land kwa mwaka mzima na hadi sasa kampuni inadai dola za Marekani 36,000,” anadai Wiston.
 
Anadai kilichomsikitisha zaidi ni pale mke wake alipoondoka mwaka 2006 na kutorudi nyumbani kuulizia watoto wanaendeleaje hadi sasa na sasa amejitokeza na kutaka apatiwe watoto na mali.
 
Winston anadai baraza lilishauri ndoa hiyo ivunjwe kwa sababu ya kutengana miaka mitano na kuamuru watoto watatu ambao ni Sifael Wiston, Anna Wiston na Joshua Wiston, wakae kwa baba yao na mama awe huru kuona watoto wake.

Post a Comment

 
Top