“Tunachokitaka ni kuunganisha nguvu zetu ili
kuhakikisha tunaing’oa CCM madarakani kwanza, masuala mengine kuhusu
ruzuku tutaweka utaratibu maalumu baadaye,” alisema.
Profesa Lipumba ambaye pia ni mwenyekiti mwenza wa
Ukawa, alisema hayo Dar es Salaam jana alipokuwa akiwaeleza waandishi
wa habari maazimio ya Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la CUF lililokutana
Jumatatu na Jumanne iliyopita.
“Wenzetu Kenya waliweza kuungana na kuhakikisha
wanaking’oa chama tawala madarakani, lakini sasa kwa hapa mkiungana na
kuwa chama kimoja ni lazima msajili chama chenu, sasa tunachokitaka ni
kushirikiana tu kwanza,’’ alisema.
Alisema suala la ruzuku na uteuzi wa viti maalumu
siyo lengo kuu la Ukawa inayoundwa na vyama vinne; CUF, Chadema,
NCCR-Mageuzi na NLD kwa kuwa linajadilika. Alisema jambo la msingi hivi
sasa ni ushirikiano wa amani.
Alisema kinachotakiwa kwa viongozi wa Ukawa ni
kuaminiana kwanza ili kulinda muungano huo ambao alisema umeshaanza
kukitikisa chama tawala, CCM.
Maazimio ya Baraza Kuu
Alisema Baraza hilo lilisisitiza umuhimu wa
kuaminiana miongoni mwa vyama washirika katika ngazi zote ili kudumisha
umoja huo na kufikia lengo la kuitoa CCM madarakani.
“Baraza limetaka uwepo utaratibu mzuri na wa wazi
utakaoonyesha mambo ya msingi ambayo vyama vinavyounda Ukawa
vimekubaliana. Utaratibu huu uwafikie viongozi wa ngazi zote za chama
ili kuhakikisha jukwaa la Ukawa linatumika kwa lengo na dhamira iliyopo
ndani ya hati ya makubaliano ambayo ni kuing’oa CCM madarakani,”
alisema.
Kuhusu uchaguzi wa Serikali za Mitaa Profesa
Lipumba alisema Baraza limetaka sheria irekebishwe ili uchaguzi wa
diwani ufanyike pamoja na wa viongozi wa mitaa, vijiji na vitongoji kwa
wakati mmoja, kwa vile diwani ndiye kiongozi mkuu wa kuchaguliwa wa
kata.
Baraza hilo pia limetaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi
(NEC), iratibu na kusimamia uchaguzi wa Serikali za Mitaa na
utengenezwe utaratibu ambao utaifanya Tume hiyo kuwa huru kuwezesha
chaguzi zote zijazo kufanyika kwa uhuru na haki.
“Taarifa za Tume zilieleza kuwa itaandikisha
wapigakura mpaka kwenye ngazi ya vijiji na vitongoji, kwa hiyo uchaguzi
wa Serikali za Mitaa usubiri mpaka daftari la kudumu la wapigakura
likamilike na ndilo litumiwe kwenye uchaguzi huo,” alisema.
Akizungumzia Katiba Inayopendekezwa, Profesa Lipumba alisema
Baraza Kuu la CUF, limesikitishwa kwa kiasi kikubwa na kitendo cha
kupitishwa na kutangazwa kwa katiba hiyo na Bunge la Katiba
lililoongozwa na Samuel Sitta akisema halikuzingatia sheria na taratibu
za mabunge ya Jumuiya ya Madola.
“Ni ukweli usiofichika kwamba mchakato mzima wa
kupitisha katiba haukuwa na mwafaka wa kisiasa, kanuni za uendeshaji wa
bunge hilo zilikiukwa na Katiba yote inayopendekezwa haikupigiwa kura ya
mwisho,” alisema
Profesa Lipumba alisema, katika vikao vya
ushauriano na viongozi wa vyama vya siasa vinavyounda Kituo cha
Demokrasia Tanzania (TCD), Rais Jakaya Kikwete alikubaliana na viongozi
hao kuwa mchakato wa kupata Katiba Mpya, hususan kura ya maoni
uahirishwe mpaka baada ya Uchaguzi Mkuu 2015.
“Mwanasheria wa Serikali alitangaza kura ya maoni
Machi 30, Rais akiwa China alisema Aprili, yaani tayari tarehe
imeshatangazwa kabla hata ya daftari la wapigakura kukamilishwa,”
alisema.
Alisema baraza hilo pia limesikitishwa na
utaratibu unaofanywa na NEC juu ya uboreshaji wa Daftari la kudumu la
Wapigakura akisema hadi sasa hatua za uandikishaji hazipo wazi na wadau
wengi hawana taarifa za kutosha juu ya nini kinaendelea.
Alisema takwimu za Sensa ya Watu na Makazi 2012,
zinaonyesha kuwa kuna vijana zaidi ya milioni 4.6 ambao watafikisha umri
wa kuwa wapigakura kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2015 lakini bado
hawajapewa fursa ya kuandikishwa huku wananchi wengi wakiwa
wameshapoteza vitambulisho vya kupigia kura.
Alisema Juni, 19 mwaka huu, Nec, ilitangaza kufuta
matumizi ya vitambulisho vya kupigia kura vya sasa na badala yake
itatumia teknolojia mpya ya Biometric Voter Registration (BVR), ikiwa ni
maboresho ya daftari la kudumu la wapiga kura na kwamba Mwenyekiti wa
Nec, Jaji Damian Lubuva alinukuliwa akisema katika Kura ya Maoni ya
Katiba na Uchaguzi Mkuu, mpigakura atatumia kitambulisho kipya baada ya
kuandikishwa upya katika mfumo huo na si vinginevyo.
Pia alisema Baraza Kuu linalaani vitendo vya
uvunjifu wa haki za binadamu na sheria vinavyoendelea kufanywa na
Serikali kwa kulitumia Jeshi la Polisi.
Alitoa mfano wa masheikh waliokamatwa Zanzibar na
kuhamishiwa Dar es Salaam na kufunguliwa kesi akisema walijitokeza mbele
ya Mahakama na kusema waziwazi kwamba wamefanyiwa mateso na vitendo vya
kinyama lakini hakuna hatua zilizochukuliwa ikiwamo kupelekwa
hospitali.
Kadhalika, alisema baraza hilo limepokea kwa
mshangao taarifa za utoaji wa uraia unaofanywa na Serikali kipindi hiki
cha kuelekea kwenye uchaguzi. Alisema uamuzi wa kuwapa uraia wakimbizi
katika majimbo yanayoongozwa na wabunge wa vyama vya upinzani ni mbinu
ya kudhoofisha upinzani kwa kuwa wakimbizi wanaopewa uraia
wanahamasishwa kuwa wachague chama tawala.
Kuhusu ardhi alisema: “Pamoja na Tanzania kuwa na
ardhi ya kutosha kwa raia wake, ugawaji wa mapande makubwa ya ardhi kwa
wawekezaji yataleta mtafaruku wa uvunjifu wa amani na kuwafanya raia
wazawa kuwa maskini wa kudumu,’’ alisema Profesa Lipumba.
Kuhusu maradhi hatari ya ebola, Profesa Lipumba
alisema Baraza Kuu limeitaka Serikali kuwa makini ili usiingie nchini
akisema limesikitishwa na taarifa ya kwamba mpaka sasa nchi haina vifaa
vya kuthibitisha kuwapo kwa vimelea vya ebola.
Chanzo: Gazeti la Mwananchi
Chanzo: Gazeti la Mwananchi
Post a Comment