"Sitamwaacha binti yangu ateseke kama mimi ninavyoteseka nikiwa katika siku zangu. Familia yangu inafanya nijihisi najisi.
"Siruhusiwi kwenda jikoni, Siwezi kuingia hekaluni, Siwezi kukaa na wengine."
Kuna hisia ya dhamira katika sauti ya Manju Baluni mwenye umri wa miaka 32. Nilikutana naye katika kijiji cha Uttarakhand, jimbo lenye miinuko kaskazini mwa India.
Nchini India,kuna ukimya kuhusu suala la afya ya wanawake, hususan wawapo katika siku zao. Kuna mwiko uliojikita katika jamii hizi kuhusu suala la mwanamke awapo katika hedhi: wanawake si wasafi, wachafu, wagonjwa na wakati mwingine wamelaanika katika kipindi hicho.
'Wasiwasi na Mashaka'
Uchunguzi wa hivi karibuni wa kampuni ya kutengeneza taulo maalum za kujisitiri kina mama wanapokuwa katika hedhi umeonyesha kuwa asilimia 75% ya wanawake wanaoishi mijini bado wananua taulo hizo zikiwa zimefungwa katika mifuko au gazeti ili kutoonyesha kilichomo ndani kwa sababu ya aibu inayohusishwa na hedhi.
Na kamwe hawawaombi wanaume katika familia kuwanunulia taulo hizo maalum.
Nimekulia katika nyumba yenye wanawake wengi, lakini bado hatuwezi kujadili kwa uwazi suala hili ambalo ni la kawaida.
Wasichana wanajifunza kuficha nguo zao wanazotumia wawapo kwenye hedhi kwa wanaume baada ya kuzifua, anasema Rupa Jha. Mama yangu alitumia mashuka makuu kuu na kuzificha katika sanduku, tayari kwa kutumiwa na mabinti zake wanne.
Changamoto kubwa ni namna ya kukausha vipande hivyo vya nguo. Nina kumbukumbu za kuhisi wasiwasi na mashaka juu ya mchakato mzima.
Nilifundishwa mbinu nadada zangu wakubwa - namna ya kuficha nguo zenye madoa ya damu chini ya nguo nyingine bila ya mwanaume yeyote kugundua. Hatukuthubutu kuziacha peupe kwenye jua ili zikauke kabisa.
Nilihisi 'mchafu sana'
Matokeo ni kwamba kamwe hazikukauka vizuri, ziliacha harufu ya uvundo. Nguo hizo zisizo safi zilitumika tena na tena.
Ukosefu wa maji ulifanya kazi ya ufuaji kuwa ngumu na isiyo na usafi. Hali hiyo haijabadilika sana tangu wakati huo kwa wanawake wengi wa Kihindi.
Uchunguzi mwingi uliofanyika siku za karibuni umeonyesha kuwa mila hizi zimesababisha madhara makubwa ya kiafya. Imeripotiwa kuwa mmoja kati ya wasichana watano nchini India anaacha masomo kutokana na kadhia ya hedhi.
Baadhi ya wasichana wanaacha kwenda shule wawapo katika kipindi cha hedhi. Margdarshi mwenye umri wa miaka kumi na mitano anaishi katika kijiji cha ndani cha Uttarakashi.
Anapenda kwenda shule japo inamaanisha safari ngumu akipita katika eneo lenye vilima vikali. Kamwe hajawahi kukosa masomo, isipokuwa kwa mwaka jana wakati ambapo nusura aache masomo baada ya kupata siku zake kwa mara ya kwanza.
"Tatizo kubwa kuliko yote ilikuwa namna ya kukabiliana na hali hiyo. Bado lipo. Najisikia kufedheheshwa, hasira na mchafu sana. Mwanzoni niliacha kwenda shule."
'Suala la kibinadamu'
Anataka kuwa daktari na anashangaa kwa nini wavulana katika darasa lake wakati wa somo la elimu ya viumbe(baolojia) wanacheka sana mwalimu anapoelezea njia ya hedhi.
"Nachukia. Natamani tungekuwa huru zaidi na kujisikia huru tunapozungumzia suala hili. Hali hii inatokea kwa kila mwanamke kwa hiyo kuna nini cha kuchekesha hapo?"
Anshu Gupta, mwanzilishi wa shirika lisilo la kiserikali, Goonj, anahisi kuwa tatizo hili limejikita katika ukweli kwamba linahusishwa na wanawake.
Nchini India wanawake wanatumia taulo za kujihifadhi wakati wawapo katika siku zao kwa kutumia nguo kuu kuu. "Si suala la wanawake pekee. Ni suala la kibinadamu lakini tumelibagua. Baadhi yetu tunataka kuondokana na utamaduni huu wa kuona aibu na kunyamaza. Tunahitaji kuvunja utamaduni huu."
Shirika hili linafanya kazi katika majimbo 21 kati ya 30.
Shirika hili pia linatengeneza taulo rahisi kutokana na nguo zilizochakatwa upya ili kuwasaidia asilimia 70% ya wanawake wa India ambao hawawezi kupata taulo salama na safi.
Muhimu zaidi, wanaanza kuzungumzia suala hili. Bila kuhisi kufedheheka.
BBCSWAHILI
Post a Comment