Kafulila
alikamatwa mapema jana asubuhi katika mji mdogo wa Nguruka wilaya ya
Uvinza mkoani Kigoma, ambako alikuwa akifanya mikutano ya hadhara,
kuelezea sakata la uchotwaji wa fedha katika akaunti ya Escrow na
kampeni kwa ajili ya uchaguzi wa serikali za mitaa.
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Kigoma, Jafari Mohammed amethibitisha kukamatwa kwa
mbunge huyo, ambaye anahojiwa katika Kituo Kikuu cha Polisi mjini
Kigoma.
Kamanda
huyo alisema Kafulila alikamatwa jana asubuhi na askari polisi na
kusafirishwa hadi mjini Kigoma, ambako anahojiwa kuhusu matamko ya
uchochezi aliyokuwa akitoa kwenye mikutano yake ya hadhara.
Alisema
katika mikutano yake, Kafulila aliwataka wananchi kutochangia kwa namna
yoyote ujenzi wa maabara katika shule za sekondari na kwamba viongozi
watakaokuwa wakifika kwenye maeneo yao kuhamasisha michango na ujenzi wa
maabara hizo, wawapige mawe.
“Alichokuwa
akifanya Mbunge Kafulila kwa kweli tumeona ni uchochezi na kinaweza
kusababisha kuvurugika kwa amani na hivyo tumemkamata tunamshikilia hapa
kituo kikuu mjini Kigoma, anahojiwa na maafisa wa juu wa upelelezi wa
mkoa,” alisema Kamanda huyo.
Katika
mazungumzo yake na waandishi wa habari, Kamanda Mohammed alisema kwa
leo (jana) hawakuwa na maelezo ya ziada ya hatua gani watachukua na
kwamba baada ya mahojiano jana, leo wanatarajia kutoa taarifa ni hatua
gani zitachukuliwa dhidi yake.
Kafulila
aliwasili mkoani Kigoma Jumamosi Desemba 6 mwaka huu, ambapo alihutubia
mkutano wake wa kwanza katika uwanja wa Community Centre Mwanga mjini
Kigoma kabla ya kuendelea na ziara katika vijiji mbalimbali vya wilaya
ya Uvinza.
Katika
mikutano yake, Mbunge huyo alikuwa akitumia muda wake mwingi kuelezea
sakata la uchotwaji wa fedha katika akaunti ya Tegeta Escrow, huku
akitoa shinikizo kwa serikali kutekeleza maazimio manane yaliyotolewa na
bunge kuhusu sakata hilo
Post a Comment