0
Wiki hii nimejikuta nikiongelea sana fedha, hela au mkwanja na kugundua vitu vingi ambavyo vinaendelea katika jamii zetu nje na ndani ya Tanzania. Kila mtu anahitaji fedha au hela kwa matumizi ya kila siku kutokana na uchumi wetu ulivyokaa. Changamoto ni pale ninapojiuliza je ni kiasi gani kinanitosha au kukidhi mahitaji yangu ya kila siku? Tumetofautiana na hakuna anayeweza 

kuonyesha kuridhika na kile unachopata kila siku au kila mwezi, kutokana na gharama za maisha. Suala la msingi hapa nazungumzia watu au mtu ukiabudu sana hela ni nini matokeo yake?

Ninapoandika makala hii, ninazingatia na kujua kuwa kuna watu wanaishi mazingira magumu na hawana msaada, vile vile kuna wengine ni kwamba wana tamaa tu ya maisha fulani au wanahusudu sana pesa na si kwamba wana mazingira magumu au kuishi masiha magumu yenye shida. Kuna wengine wetu tunaotaka utajiri wa fasta fasta ili tuweze kuendana na watu ambao wanatuzunguka au jamii ya marafiki kwakuwa wana uwezo kiasi fulani au vile vile unataka watu tu wakuone kwamba na wewe unazo. Je unahusudu hela kwa kiasi gani?
Fedha ni jawabu ya mambo yote lakini si kwa kila kitu, ndio maana hata matajiri wanakufa ingawa wana hela hiyo hiyo. Kuna vitu vya msingi ambavyo kila mtu atahitaji kuwa na hela ili vifanyike, kiwango ninachotaka kukiongelea hapa ni pale ambapo mtu amevuta amehitaji ya msingi kama chakula, mavazi na malazi. Inamaanisha mtu huyu ana uwezo wa kusoma au amesoma na ana kazi nzuri au kipato kizuri na maisha yanaendelea mbele tatizo anahusudu hela au fedha.
Kupenda kwetu fedha kunasababisha maadili na malezi ya familia kupotea au kuharibika kabisa. Hili jambo linazikumba familia zetu kiasi kwamba hakuna tena malezi mazuri kwani kila mtu kwenye familia anatafuta hela na kuwafanya watoto kuishi kana kwamba hawana wazazi. Hawajui wajifunze wapi maisha au maadili, fedha hiyo hiyo inatufanya tutafute vitu visivyo vya msingi na kuacha vitu vya msingi. Hivi kwani ni shilingi ngapi ukikusanya italea na kumpa maadili mazuri mtoto?
Watu wanauawa kwa sababu ya Pesa. Hivi karibuni tunaendelea kushuhudia uhalifu mkubwa kwa vijana wanaotumia pikipiki na silaha za moto bila hata woga au huruma wakiua watu kisa wanatafuta pesa. Ingawa watu wengine wamekuwa wakisema ni kwasababu ya uzembe wa hao wanaobeba pesa na kutembea nazo na wanasahau kwamba kwenye ulimwengu huu wa nchi hii ya Tanzania bado biashara nyingi zinafanyika kwa pesa taslimu zaidi kuliko kadi kwenye nchi zilizoendelea.
Wengine wanajikuta wakijiingiza kwenye biashara au matendo ya aibu ilimradi tu wapate pesa na kuongeza umaarufu. hii inawakumba wengine kujihusisha na rushwa, kujiuza na biashara halafu ili kupata fedha nyingi na za haraka kwa muda mfupi bila kujali usalama wao na thamani yao ya maisha. Kama umekuwa mkazi wa kinondoni, vijana wengi wamepotea na hawajaweza kurudi nchini baada ya kukamatwa na madawa ya kulevya ughaibuni, na familia nyingi hapa Dar es Salaam ni wahanga wa vijana hao. Katika dunia hii hakuna namna utakakwenda kwa njia za mkato na ubakie salama, kuna gharama ya kulipa na lizima ilipwe kwa wewe kuhusudu hiyo pesa.
Kitu ambacho nimejifunza Jumahili lililopita ni kutumia chini ya kipato kile unachopata na kupanga katika hicho kipato na si zaidi, kutakupunguzia matatizo mengi. Ukweli mwingine ni kwamba ukifanya kwa usahihi huwezi kujutia maamuzi yako ya kila siku, ukienda kwa pupa zaidi na hatari ya kuharibikiwa au kupotea ni rahisi zaidi. Waswahili wenyewe wanasema mwenda pole hajikwai na haraka haraka haina baraka, kazi ni kwako kusuka au kunyoa.

Post a Comment

 
Top