Meneja Uhusiano na Masoko
wa Mfuko wa Pensheni wa PPF, Lulu Mengele, akitoa mada kuhusiana na
huduma mbalimbali zitolewazo na Mfuko huo kwenye semina iliyoandaliwa na
Mfuko huo kwa wanafunzi wa mwaka wa mwisho Chuo Kikuu cha Dodoma
(UDOM), ambapo zaidi ya wanafunzi 500 walihudhuria semina hiyo Jumamosi
Machi 29, 2014.
Baadhi ya wanafunzi wa
Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), wakifuatilia mada kutoka kwa Meneja
Uhusiano na Masoko wa Mfuko wa Pensheni wa PPF, Lulu Mengele.
Meneja wa Kanda ya
Mashariki na Kati wa Mfuko wa Pensheni wa PPF, John Mwalisu, akitoa mada
kwenye semina ya siku mbili, iliyoandaliwa na Mfuko huo kwa wanafunzi
wa Chuo kikuu cha Dodoma (UDOM).
Baadhi ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), wakifuatilia mada.
WANAFUNZI wa mwaka wa mwisho wa Chuo
Kikuu cha Dodoma (UDOM), wameridhishwa na mada mbalimbali zilizotolewa
na Mfuko wa Pensheni wa PPF, na wameahidi kujiunga kwa wingi na Mfuko
huo, kwani wengi wao wanatarajia kujiajiri, hivyo itakuwa fursa nzuri
kwao kuandaa maisha yao ya baadaye watakapostafu.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti chuoni
hapo jana mara baada ya semina iliyoandaliwa na PPF kwa wahitimu wa
elimu ya juu, walisema awali walidhani kwamba Mfuko wa Pensheni wa PPF
ni kwa ajili ya wafanyakazi walioajiriwa tu, lakini sasa wamefahamu kuwa
milango iko wazi hata kwa wale ambao wamejiari ili mradi tu wawe na
umri wa kuanzia 18.
Mmoja wa wanafunzi hao, Oneck Mwalongo,
alisema kwa muda wote ambao amekuwa chuoni alikuwa hajawahi kuona
maofisa wa mifuko inayojihusisha na masuala ya hifadhi ya jamii wakifika
kwa ajili ya kuwapa semina kuhusiana na fursa zinazotolewa, lakini PPF
imekuwa ya kwanza kuwapa elimu hiyo.
"Lakini leo hii tunashukuru PPF
wametufumbua macho kwani tulikuwa tunajua ili uwe mwanachama ni lazima
uwe umeajiriwa, kwangu mimi nitajiunga na PPF kwa sababu kozi yangu ya
sayansi ya kompyuta si lazima niajiriwe nitajiajiri mwenyewe," alisema
Mwalongo.
Alisema mfumo wa uwekaji amana wa hiari ulioanzishwa na PPF utasaidia vijana wengi watakaokuwa wamejiajiri kujiwekea akiba.
Pia alisema amefurahishwa na mpango wa
baadaye wa PPF wa kuanza kukopesha wanachama wake viwanja, kwani nyumba
ndiyo jambo muhimu kwa maisha ya binadamu.
Mwalongo, alisema wakati akiingia kwenye
semina hiyo alikuwa hafahamu kama maisha ya kesho huanza kuandaliwa
leo, hivyo atakapoondoka chuoni hapo ataanza kujiwekea akiba ili
asikumbane na msemo wa fainali uzeeni.
"Nilikuwa sifahamu kama maisha ya kesho yanaandaliwa leo wamenionesha njia sasa naanza kuandaa maisha ya uzeeni," alisema.
Kwa upande wake, Elizaberth Elibarick,
alisema PPF ni mfuko wa kujiunga nao hasa kwa kuzingatia mfuko huo una
mfumo wa uwekaji amana wa hiari na unatoa fao la elimu kwa watoto wa
mwanachama anapofariki akiwa bado kazini.
Alisema si jambo la mchezo Mfuko
kumsomesha mtoto au watoto wa wanachama ambao wamefariki kuanzia darasa
la awali hadi kidato cha sita na kizuri zaidi wanalipa mafao kwa
wakati.
Naye Leonard Mgeja, alisema kupitia
semina hiyo yeye na wanafunzi wenzake wameweza kufahamu vitu vya msingi
ambavyo walikuwa hawafahamu kuhusiana na Mfuko wa PPF.
"Leo tumefahamu umuhimu wa maandalizi ya
maisha ya baadaye tukiwa na umri mdogo ili kufanya mambo sahihi kabla ya
kufikia uzeeni," alisema na kuongeza kwamba;
"Hivi sasa ambapo tunakaribia kwenda
makazini tunaenda na mwanzo mzuri kwani hatutegemei kuajiriwa tu, bali
na kujiajiri hivyo tutajiunga na uchangiaji wa hiari kama hatutakuwa
kwenye mfumo rasmi wa ajira."
Awali Meneja Uhusiano na Masoko wa Mfuko
huo, Lulu Mengele, aliwaasa wanafunzi hao wa mwaka wa mwisho zaidi ya
500 waliohudhuria semina hiyo, kujiunga na PPF kupitia Mfumo wa asili wa
Pensheni au ule wa uwekezaji amana pale ambapo wataamua kujiajiri
wenyewe.
“Mfumo wa uwekezaji amana, unaandikisha
watu kutoka sekta isiyo rasmi, kama wakulima, wafugaji, machinga na mama
lishe”. Alifafanua.
Katika mada ya uwekezaji amana, Lulu alisisitiza umuhimu wa kuweka akiba kwani matayarisho ya maisha ya kesho yanaanza sasa.
Kwa upande wake Meneja wa Mfuko wa
Pesnheni wa PPF, Kanda ya Mashariki na Kati, inayojumuisha Mikoa ya
Morogoro, Dodoma na Singida, John Mwalisu, alisema PPF imeandaa semina
hiyo kwa wanafunzi wa mwaka wa mwisho wa chuo hicho kwa kuwa wao ndiyo
wanaingia kwenye soko la ajira.
Alisema kutokana na wao kuwa na nguvu ya
kuajiriwa au kujiajiri wameona ni vema kuwaelimisha namna nzuri ya
kutunza akiba ili iwasaidie watakapokuwa fikia hatua ya kustaafu.
Post a Comment