0


Jeshi la Polisi Mkoani Mbeya limewafukuza kazi Askari 6 wa kikosi cha Usalama barabarani  Wilaya za Rungwe na Mbeya kwa tuhuma za kuomba,kushawishi na kupokea rushwa.

Kamanda wa Polisi  Mkoani Mbeya  Ahmed Msangi amewatataja Askari hao kuwa ni pamoja na waliokuwa wakifanya kazi wilaya ya Mbeya barabara ya Mbeya/Tunduma eneo la Songwe  ambao ni Copro Jonson,PC Rymond na PC Simon.

Msangi amewataja wengine kuwa ni pamoja Sajini Hezron,PC Shaban na PC Kajolo ambao walikuwa wanafanya kazi barabara ya Mbeya/Rungwe wilaya ya Rungwe.

Askari hao walikuwa wanakabiliwa na makosa hayo na walifikishwa katika Mahakama ya Kijeshi na Hukumu kutolewa Aprili 24 mwaka huu kwa  kupewa adhabu ya kufukuzwa kazi.

Aidha Kamanda Msangi amesema Jeshi lake halitasita kuwafukuza kazi Askari watakaokwenda kinyume na maadili ya Jeshi la Polisi na Askari yeyote atakayekwenda kinyume atakumbwa na adhabu kali ikiwa ni pamoja na kufukuzwa kazi au kufikishwa mahakamani.

Askari wengine waliofukuzwa kazi hivi karibuni ni pamoja na PC James Kagomba ambaye amehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela baada ya kupatikana na hatia ya wizi wa kutumia silaha,WP Prisca Kilwai anayekabiliwa na kesi ya wizi wa mtoto.

Wengine wliohukumiwa kifungo cha mwaka mmoja baada ya kukutwa na hatia ya kuua bila kukusudia ni DC Marcelino Venance mwenye namba 8084,PC Juma Idd mwenye namba 3117 na Askari wa Mgambo MG Jackson Mwakalobo ambao walidaiwa kusababisha kifo cha mwanafunzi Dentho Kajigili aliyekuwa mwanafunzi wa shule ya Sekondari Ivumwe ya Jijini Mbeya.

Credit: Mbeya yetu blog


HABARI KAMILI..>>>

Trafiki afia ndani ya daladala aliyoikamata mkoani Kilimanjaro..."wakiwa njiani kuelekea kituoni ghafla yule trafiki akawa haongei",anasema shuhuda wa tukio hilo



Ofisa wa polisi mwenye cheo cha Koplo, Wilson Mwakipesile wa Kikosi cha Usalama Barabarani mkoani Kilimanjaro amefariki dunia ghafla akiwa ndani ya daladala alilokuwa amelikamata. 
 
Hata hivyo, haikujulikana mara moja iwapo trafiki huyo alifariki dunia akiwa njiani kulipeleka gari hilo kituo cha polisi, alifariki muda mfupi baada ya kufika kituoni au wakati anapelekwa hospitali.
 
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Robert Boaz alisema polisi huyo alikufa ghafla akiwa kazini lakini alikataa kuingia kwa undani wa tukio hilo lilitokea Ijumaa kati ya saa 5:00 asubuhi na saa 6:00 mchana, baada ya trafiki huyo kukamata daladala linalofanya kazi zake kati ya Kiborloni na katikati ya mji.
 
Mmoja wa mashuhuda alisema :“Baada ya kuikamata hiyo Hiace (Toyota) pale Kiborloni aliingia kwenye hiyo gari na kukaa kiti cha mbele pembeni ya dereva na kumwamuru kulipeleka kituoni.
 
“Wakati wakiwa njiani kuelekea kituoni ghafla yule trafiki akawa haongei na akawa anamwegemea dereva… hiyo hali iliendelea hadi walipofika kituoni ndipo dereva akawaeleza trafiki wenzake.” 

Mwili wa polisi huyo ulisafirishwa juzi kwenda Mbeya kwa mazishi.


HABARI KAMILI..>>>

Monday, April 28, 2014

Majambazi yahukumiwa kifungo cha miaka 270 Jela wilayani Chunya mkoani Mbeya



Mahakama ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Chunya mwishoni mwa wiki iliwahukumu watu tisa kwenda jela jumla kwa miaka 270 baada ya kupatikana na hatia ya wizi wa kutumia silaha. 
 
Washtakiwa hao ni Samweli Sarehe (40), Bahati Kenson (29), Aulesi Andason (28) na Ayubu Swila (24), wote wakazi wa Mbalizi  Wilaya ya Mbeya Vijijini.
 
Wengine ni Mathias Simfukwe (31), Pascal Simchimba (27) wote wakazi wa  Kijiji cha Kanga Wilaya ya Chunya, Tegemea Kenya (27) mkazi wa Kijiji cha Mjele, Shukuru Mwakatumbula (27) wa Ifumbo na Maleba Kindagilo (46) wa Lupa, Chunya.
 
Awali, ilielezwa mahakamani hapo na mwendesha mashtaka wa polisi, Raymond Lukomwa kuwa washtakiwa  wote kwa pamoja walifikishwa mahakamani hapo Desemba 27, 2013 kwa kosa moja la wizi wa kutumia silaha  kinyume na Kifungu cha 287A cha Sheria ya Adhabu, Sura ya 16 iliyofanyiwa marekebisho 2012.
 
Alidai kuwa washtakiwa walifanya kosa hilo Desemba 14, 2013 katika eneo la Kasangakanyika ambako waliiba vipimo vitano vya dhahabu vyenye thamani ya Sh58 milioni na fedha tasilimu Sh6milioni, mali ya Paul Sinjale (44) na kwamba katika wizi huo walitumia bunduki aina ya shortgun.
 
Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Mkazi wa Wilaya ya Chunya, Desdeli Magezi alisema kwa mujibu wa Kifungu cha Tano (A) (ii) cha Sheria ya Adhabu, Sura ya 90 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002 wote kwa pamoja wanahukumiwa kifungo cha miaka 270 na kila mmoja atatumikia kifungo cha miaka 30 jela.

Post a Comment

 
Top