0


Watu 15 wamejeruhiwa kutokana na mlipuko wa bomu katika baa maarufu ya Arusha Night Park katika eneo la Mianzini katika jiji la Arusha.
 
Tukio hilo lilitokea jana saa mbili usiku wakati mamia ya watu wakiwa katika baa hiyo wakiangalia  mechi ya soka ya Ligi Kuu ya England kati ya Chelsea na Swansea. Chelsea ilishinda 1-0.
 
Mmoja wa wamiliki wa baa hiyo, Angelo Mwoleka pia alithibitisha kutokea mlipuko huo na kueleza kujeruhiwa watu kadhaa.
 
“Ni kweli kuna mlipuko umetoka na watu kujeruhiwa, mimi sikuwepo ila nipo njiani nakwenda eneo la tukio, “alisema.
 
Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo, John Lymo alisema watu saba waliumia vibaya kutokana na bomu hilo na walipelekwa katika Hospitali ya Mkoa Arusha ya Mount Meru.
 
Akizungumzia tukio hilo,  Mkuu wa mkoa wa Arusha, mh. Magesa Mulongo, ambae ni kiongozi wa Kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa  amesema  watu 15 wamejeruhiwa kwenye mlipuko huo.

Amesema   majeruhi  wote wamepelekwa hospitali ambapo uchunguzi wa awali umeonyesha  kuwa bomu hilo ni la kutengenezwa kwa mkono na mpaka sasa hajajulikana alietekeleza shambulio hilo.

Mulongo  pia amesema hakuna  mtu aliyepoteza maisha kwenye shambulio hilo ambalo uchunguzi wa awali umeshatoka, ila baadae itatoka taarifa rasmi pale uchunguzi kamili utakapokamilika.
 
Tukio hilo limekuja wakati bado jiji la Arusha likiwa na kumbukumbu ya kushambuliwa kwa mabomu kwa Kanisa la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi lililopo eneo la Olasiti  na jingine Uwanja wa Soweto wakati Chadema walipokuwa wakifunga kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani. 

Katika matukio yote hayo, watu sita waliuawa na wengi kujeruhiwa.

Post a Comment

 
Top