0
Yobnesh Yusuph'Batuli'.

NI nadra sana kumkuta akiwa amenuna. Sura yake mara zote ni yenye tabasamu, uso wake una nuru na ang’avu wakati wote. Macho yake ni kivutio kingine kwa mrembo huyu. Weka yote pembeni, kutana naye akiwa nyuma ya kamera utamkoma! Maneno ya kuanisha sifa zake ni mengi.

Naweza kuandika ukurasa mzima, lakini hayo yatoshe kueleza ubora wa mwananadada huyu katika uhalisia na uigizaji. Ni Batuli.
Jina lake halisi ni Yobnesh Yusuph, 28, mama wa watoto wawili, wavulana – Samir na Malima. Katika mazungumzo na Risasi Mchanganyiko, Batuli amezungumza mengi kuhusu maisha yake na changamoto anazokutana nazo kwenye sanaa.
Kwanza nilitaka kujua kwa nini kumekuwa na migogoro ya wasanii wa kike kuchukuliana mabwana? Huyu hapa anafafanua: “Wanaoweza kufanya hivyo ni wenye tabia za aina hiyo tu. Ni kweli kuna hiyo tabia miongoni mwetu lakini kiukweli inashusha sana heshima.
“Matokeo yake sasa, hata sisi ambao hatuna tabia hizo, tunawekwa kwenye mkumbo mmoja. Lakini sababu hasa ninayoiona ni tabia ya sisi wanawake kutambiana. Mtu akiwa anatoka na mwanaume fulani anaanza kumwanika na kueleza sifa zake.
“Sasa waroho ndiyo wanapoanza kummendea na wakimkwapua, inakuwa imekula kwako. Ndiyo maana mimi nimeamua kamwe sitamweka wazi mwanaume ninayetoka naye hadi itakapofikia hatua ya ndoa. Ni kwa sababu naogopa majanga kama hayo.”

Vipi maisha yako ya ndoa?
“Niliwahi kuishi na mume wangu wa ndoa, tukafanikiwa kupata mtoto mmoja, lakini baadaye ilibidi nidai talaka. Niliishi kwenye ndoa ya manyanyaso sana. Mume wangu alikuwa akinisaliti waziwazi kiasi kwamba alifikia hatua akawa anatoka na marafiki zangu wa karibu.
“Nilishindwa kuvumilia, nikaomba talaka. Nashukuru tuliachana salama. Kwa sasa mwanetu anakaa ukweni (kwa wazazi wa mume) na mimi naendelea na maisha yangu. Baada ya kutengana naye nilikutana na mwanaume mwingine ambaye naye nilizaa naye mtoto mwingine.”
Unaishi naye mpaka sasa?
Naomba hilo nisilifafanue. Niulize maswali mengine tafadhali.

Vipi penzi lako na Mwakifwamba?
“Nimesikia kuhusu hilo. Nimelisoma kwenye magazeti. Ukweli ni kwamba, hatuna uhusiano. Namheshimu kama bosi wangu (Rais wa TAFF) na kaka yangu.
“Tupo karibu kikazi, kuna wakati nilisafiri naye pamoja na Monalisa (Yvon Cherry) kwenda Dodoma kwenye Bunge Maalum la Katiba, basi yakaenezwa hayo. Wasanii hatupendani, ndiyo maana wakasambaza hayo maneno ya uongo.”
Ila ushahidi upo, hata Mwakifwamba mwenyewe anakiri!
“Aaah! Wapi? Hata tukimpigia sasa hivi hapa, nikaweka simu loud speaker, utasikia neno lake la kwanza kuniambia ni nini. Sina uhusiano naye kabisa. Halafu maskini, Mwakifwamba mwenyewe, hata siku moja hajawahi kunitamkia hilo neno.”

Vipi kuhusu uchafu wa wasanii location?

“Halina ubishi hilo. Location yanafanyika mambo ya hovyo sana. Kifupi ni kweli, sina haja ya kuliongea sana lakini mimi nawashauri wasanii wenzangu na hasa wa kike, tujitambue jamani. Mwanamke ana thamani kubwa, tuache ujinga. Wakati unapita.”

Soko la filamu likoje?

“Ukweli soko bado gumu, ndiyo maana tunahangaikia katiba ijayo itambue sanaa kama sekta rasmi ya ajira. Filamu zinaingizia fedha nyingi sana taifa, lakini tume sahauliwa. Hata hivyo, namshukuru Mungu naweza kuendesha maisha yangu.
“Pamoja na changamoto zilizopo nina mpango wa kujitanua kimataifa. Unajua sisi wasanii hatuna fikra za mbele, tunafikiria hapa tulipo tu. Mfano marehemu Steven Kanumba aliona mbali sana, ingawa mwanzo watu walimcheka, eti hajui Kiingereza lakini alijitahidi na mpaka amefariki alituacha tumeanza kujulikana kimataifa.
“Kanumba alikuwa na moyo wa kipekee sana. Sijawahi kukutana na binadamu wa aina yake. Amesaidia wengi sana kwenye filamu nikiwemo mimi. Mungu ampumzishe kwa amani.”

Msoto kwenye game

“Nilianza zamani sana sanaa, nilijiunga na Kundi la Kaole wakati huo linawika. Niliingia na Davina (Halima Yahaya), Johari (Blandina Chagula), Kanumba na wengineo, lakini sikufanikiwa kupata nafasi kwenye tamthiliya za ITV, nikaamua kuondoka.
“Nilikaa nje ya fani kwa muda mrefu, nikifanya kazi nyingine za kuajiriwa. Nilikuwa sekretari kwenye kampuni moja. Baadaye Kanumba alinifuata na kuniomba nicheze sinema ya O’prah, hapo ni baada ya kucheza Mkasa, ambayo haikujulikana sana.
“Nilitakiwa nivae uhusika wa O’prah. Nilipopewa script na kuangalia uhusika wangu, nilikataa – ilikuwa na love scenes (vipande vya kimahaba) nyingi sana, tena zile deeply (ndani) kabisa. Baadaye nafasi yangu ilichukuliwa na msanii mwingine. Mwaka 2007, Kanumba akaniita tena, nikashiriki Fake Smile na Aunt Ezekiel na wengineo. Hapo ndipo Batuli alipozaliwa kisanii.”

Eti kuna wasanii wa kike wavuta bangi?
“Halina ubishi hata kidogo, wapo wengi sana. Wanajulikana. Kiukweli si tabia njema kwa kioo cha jamii, tena mwanamke. Ushauri wangu kwao, waache.”

Umewahi kutoa mimba?
“Mh! Wewe... hapana bwana. Ndiyo maana nina watoto wawili. Ningekuwa naua watoto, nadhani nisingekuwa nao.”

Post a Comment

 
Top