0
Mjumbe wa Bunge la Katiba, Almas Maige amesema endapo wajumbe wa Bunge hilo watapitisha muundo wa Serikali tatu, nchi itaingia katika kitabu cha maajabu ya dunia cha Guiness Book of Records.

“Hili litakuwa shirikisho la pekee hapa duniani lenye marais wengi katika nchi mbili, linaweza kuingia katika kitabu cha maajabu cha Guiness kwa kuwa na marais wengi katika nchi maskini sana,” alisema.

Mjumbe huyo alisema amejaribu kufuatilia hoja za wanaounga mkono muundo huo na kufananisha na nchi za Marekani na Nigeria, lakini akasema katika nchi hizo Rais wa nchi ni mmoja.

“Mimi nimejaribu kuwafuata wanaofananisha na Marekani na Nigeria, wameshindwa kusema katika nchi hizo mbili Rais ni mmoja tu hakuna wingi wa Rais kutokana na majimbo,” alisisitiza.

Katika hatua nyingine, mjumbe huyo aliwashangaa wajumbe wanaotokana na kundi la Ukawa kujigeuza kuwa wachunguzi wa kijinai kwa kuhoji uhalali wa saini ya muasisi wa Muungano, Abeid Aman Karume.

“Mimi nawashangaa sana wanasiasa hawa na wanasheria wa Ukawa wamejigeuza Forensic Expert (wachunguzi wa jinai). Mimi ningewaunga mkono kama wangeenda kuwauliza watoto wa marehemu,” alisema.

Aliongeza kusema: “Watoto wa marehemu wapo Zanzibar… Yupo Aman Karume aliyekuwa Rais wa Zanzibar na yuko Balozi Ali Karume na yuko pia mama Karume. Kwa nini hawawaulizi,” alihoji.

“Mimi ningefurahi sana kama wangeenda kuwauliza wanafamilia sahihi hii ni ya baba yenu? Au je, mheshimiwa mama hii ni sahihi ya mumeo? Wangekataa ndipo tungewaunga mkono,” alisisitiza.

Mjumbe huyo alisema kinyume chake, Ukawa wanavaa gamba la elimu ambayo hawana na vilevile hawajui maana na tafsiri sahihi iliyoandikwa miaka 50 iliyopita.

“Taaluma ya sasa ingeweza kugundua wino uliotumika una umri gani na kuondoa kero hiyo kama ni ya juzi au jana au kama imeghushiwa,” alisema mjumbe huyo na kuongeza kusema:

“Wataalamu wa Forensic (uchunguzi wa kijinai) wangeweza kugundua wino huo una miaka 50. Wanafanya kitu ambacho hawakijui na wanadhalilisha Watanzania.”

Mjumbe huyo alisema yeye anaunga mkono muundo wa Muungano wa Serikali mbili na kuwa Serikali tatu ni sawa na mtu kunywa sumu.

Post a Comment

 
Top