Jeshi la Polisi limepata pigo kutokana na askari wake wawili kuuawa kwa kupigwa risasi na majambazi...
Askari wawili wa jeshi hilo waliuawa kwa kupigwa risasi na majambazi katika Tarafa ya Usoke wilayani Urambo mkoani Tabora.
Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Suzan Kaganda, alisema jana kuwa tukio
hilo lilitokea juzi saa 2:30 usiku katika kijiji cha Usoke.
Kamanda Kaganda aliwataja askari waliouawa kuwa ni PC Shaban namba G
3388 ambaye alikufa papo hapo baada ya kupigwa risasi na majambazi hao
na PC Jumanne namba F.5179 aliyejuruhiwa tumboni na baadaye kufariki
dunia jana asubuhi katika Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Tabora Kitete
wakati akipatiwa matibabu.
Kamanda Kaganda alisema majambazi watatu walivamia nyumbani kwa
mfanyabiashara, Ibrahim Mohamed, mkazi wa Usoke kisha kupora fedha
tasilimu Sh. milioni 1.2. Mbali ya kufanya uporaji huo, yalipora vocha
za simu zenye thamani ya Sh. 120,000.
Alisema baada ya askari hao kupata taarifa ya uharifu huo, walienda eneo
la tukio kwa ajili kutoa msaada, lakini wakiwa mita chache kabla ya
kufika katika eneo la tukio, walikutana na majambazi hao na kuanza
kuwafyatulia risasi kwa kasi na kumuua PC Shaban.
“Ndugu zangu waandishi wa habari hili ni pigo kubwa sana kwa Jeshi la
Polisi, lakini naapa kuwasaka hadi kuwakama wakiwa hai au wafu, sasa
tumechoka na uharifu huu,” alisema Kaganda.
Kamanda huyo alisema kabla ya tukio la mauaji ya askari hao, majambazi
hao yalifyatua risasi hovyo hewani mfululizo kwa lengo la kuwatisha raia
na kwamba maganda 25 ya risasi aina ya SMG na SAR yaliokotwa katika
eneo la tukio.
Kufuatia tukio hilo jeshi la Polisi mkoani Tabora linaendesha msako na
tayari watu watano wametiwa mbaroni kuhusiana na tukio hilo.
Post a Comment