Ukweli ni kuwa watu wawili wanapoamua kwa dhati kuwa katika mahusiano ni kwamba wanakuwa tayari katika akili zao wamejenga matarajio au matumaini ya kunufaika na uhusiano husika, hata kama hawawezi ambiana moja kwa moja kuwa “ aisee, mie kuwa na wewe nataraji moja , mbili, tatu….”.
Kunapokuwepo
na upendo, basi pia kunaleta majukumu, ambapo bila ya kutimizwa kwa majukumu
yanayotarajiwa kutimizwa, maana halisi ya mahusiano bora inapotea.
Hii
si tuu kwa mahusiano ya kimapenzi, bali hata dini zinatufundisha kuwa Mungu
anatupenda, na katika hilo, tunajukumu la kutii amri zake, na kwamba tusipotii
amri zake, tunakuwa tumeharibu maana nzima ya upendo wake, kwani tutajikuta
tumeingia motoni/jehanamu (Kinyume cha upendo).
Hata
katika familia, tumesikia mzazi pamoja na upendo alioonyesha kwa mtoto wake
toka yupo tumboni mpaka mtoto ameweza kujitegemea, endapo mtoto husika
akashindwa kumjali ( hili ndio jukumu linalokuja na upendo wa mzazi), basi
unaweza sikia mzazi huyo akitoa ‘laana’ au ‘akamwachia radhi’ mtoto wake
mwenyewe wa kumzaa.
Ni
wazi kuwa mara nyingi majukumu yanayoletwa na upendo huwa hayaelezwi wazi wazi,
hata hivyo katika mahusiano, mambo yafuatayo yanaweza kuwa sehemu ya matarajio
ambayo wapenzi wanaweza kuwa makini ili
waweze kuwapendeza wenzao. Kwa maana nyingine ni kuwa yafuatayo, ndio maeneo
ambayo mtu aliye kwenye mahusiano ni muhimu ‘acheze’ vema ili kulinda
mahusiano/penzi:-
Fedha: Katika swala la fedha, jambo kubwa
linalojitokeza ni namna ya kufanya maamuzi kuhusu matumizi ya fedha. Ni muhimu kuweka mikakati ya pamoja kwa mambo
ya msingi kimaisha , na kila mmoja kutilia maanani mipango hiyo, kabla ya kuamua
kutumia kipato chake kwa mambo ambayo pengine hayapo nje ya mipango ya kifedha
ya wawili nyie kama wapenzi. Bila shaka,
kuendana na aina yenu ya kipato, aina yenu ya maisha, kama wapenzi mtakuwa na
kiwango fulani cha fedha ambacho si busara mmoja wenu kuamua kutumia bila
kumtaarifu mwenzake , hata kama matumizi husika ni muhimu sana, na haijalishi
nani kazitafuta fedha husika.
Imani: Katika swala la imani, ni muhimu
kufahamiana vema mwenendo wa kiimani wa mwenza wako, na kuheshimu kuwa swala
hili ni nyeti, na mabadiliko ya kweli hayawezi kulazimishwa. Imani inaweza
athiri namna mnavyoweza kuwasiliana kama wapenzi – kwani mwingine mwenye
msimamo mkali wa kidini, anaweza kukataa jambo fulani hapo baadae, jambo ambalo
pengine mwenza wake anaona ni jambo la kawaida tuu. Imani inaathiri malezi ya
watoto, na inaweza athiri shughuli za kiuchumi za wawili nyie, mfano pale mmoja
wenu anapoamua kujikita katika ‘huduma’
zaidi, kuliko familia na shughuli za kuingiza kipato.
Mahali pa kuishi: Mtaa gani , wilaya gani, mkoani gani, nchi
gani au bara gani kila mmoja wenu anatazamia muishi ni jambo la msingi kuliweka
wazi kati yenu. Jambo hili linaweza kuendana na mambo mengine mengi ambayo
yanachochea mabadiliko ya muda mfupi na hata muda mrefu katika maisha yenu,
kama vile , aina ya kazi mnazotarajia kila mmoja wenu kufanya, na aina ya kazi
unazotamani au kufikiri ni vema mwenza wako afanye.
Watoto: Hili ni jambo zito haswa katika
vipengele vya lini watoto wapatikane (ujauzito), idadi ya watoto, aina ya
malezi kwa watoto watakaopatikana, na zaidi sana majukumu ya kifedha katika
malezi ya watoto (mfano, nani atalipa ada ya shule, n.k). Pamoja na kutafakari
hayo, watu wawili mlio katika mahusiano, ni muhimu mkatengeneza picha ya maisha
ya watoto wenu endapo mmoja wenu atatangulia mbele za haki (atafariki), na hata
ikiwezekana mwaweza fikiria na kupanga
aina ya maisha mnayotaka watoto wenu waishi pale nyote wawili hamtokuwepo duniani. Inapotokea mambo kama hayo
yaliyotajwa hapo juu hayajawekwa wazi mbele yenu, ni rahisi mmoja wenu kufanya
mambo yasiyompendeza mwengine –mfano wakati mwingine anafikiria akiba ya baadae
ya watoto ili wakasome international school, mwingine anafikiria namna ya
kutanua ili ‘kuuza sura’.
Falsafa ya maisha: Swala hili linahusu wa kipekee na tafakari
huru ya kila mmoja wenu kuhusu mambo kadhaa ya kimaisha kama vile mtazamo wa
kila mmoja wenu kuhusu biashara (mwingine biashara ni kitu cha kuweka heshima
kwa jamii, wakati mwingine biashara ni kielelezo cha huduma kwa jamii na hivyo
kinahitaji muendelezo).
Falsafa
pia inahusu namna kila mmoja wenu anavyochukulia mambo kama vile kusaidia watu
wengine, kuwa na mahusiano na watu wa
jinsia tofauti (wapo wasiotaka hata classmet ampigie simu mpenzi wake). Falsafa
pia inahusika na namna kila mmoja anavyotafsiri mafanikio katika maisha, na alivyo
tayari kufanya yanayopaswa kufanywa kufikia mafanikio (Mfano, wengine mafanikio
ni mali na umaarufu, wakati kwa wengine mafanikio ni namna anavyoweza kuwa na
furaha na uhuru , pamoja na kusaidia wengine).
Katika
juhudi za kufikia mafanikio unawea kukuta wapenzi mnatofautiana kwani mmoja
anaweza amini rushwa ndio suluhisho pekee la kufikia anakotaka, wakati mwingine
anaamini tofauti na hivyo.
Hisia za kimapenzi: Ni jambo la msingi
kutokupuuzia hisia za kimapenzi za kila mmoja wenu. Tambua vile mwenzako
angependa akuone unamvutia na vile ambavyo unamjali hisia zake. Ni kweli kuwa
katika mahusiano, hisia za kimapenzi zinaweza zisichukue nafasi kubwa kati yenu
kwani kuna mambo mengi ya kufanya pamoja kama wapenzi, hata hivyo pamoja na
udogo wake wa muda, jambo hili nyeti lisipopewa kipaumbele, linaweza sababisha
mengine yote kuharibika. Zaidi sana, kumbuka wewe na mpenzi wako, ni watu wa
jinsia mbili tofauti, kinachowafanya muungane kiasili ni hizo hisia za mapenzi
kati yenu.
Hitimisho: Sio lazima kama watu wawili
mlio katika mahusiano muwe na mtazamo sawa katika hayo yote yaliyoelezwa hapo
juu, hata hivyo, ni muhimu sana kwenu nyote kuwa na picha kichwani ya mtazamo
wa mwenza wako kuhusu mambo hayo niliyotaja hapo juu.
Pale
mnapokubaliana kutofautiana katika
mambo yaliyotajwa hapo juu (mf.mambo ya fedha, na imani), hakikisheni mnakubaliana bila
kutofautiana kuhusu athari za kutofautiana kwenu, na jukumu la kukubali
athari hizo kwa mahusiano yenu.
Post a Comment