0

YELEUWII! Kuishi kwingi ni kuona mengi, kijana aliyejitambulisha kwa jina la Andrew Vincent (23) ambaye amemaliza kidato cha nne mwaka jana, amejikuta katikati ya matatizo kufuatia kufunga pingu za maisha na mwanafunzi wa darasa la tano aliyefahamika kwa jina moja la Wastara (12), wote wakazi wa Bagamoyo, Mkoa wa Pwani.

Wastara akifanya usafi ndani kwake baada ya kuolewa.
Tukio hilo lilijiri Aprili 26, mwaka huu ambapo kikosi kazi cha Oparesheni Fichua Maovu ‘OFM’ kilipokea taarifa kutoka kwa wasamaria wema wakilalamikia kitendo hicho na kutaka mwanafunzi huyo asaidiwe ili arudi shule.
OFM kama kawaida yake, ilitinga eneo hilo kwa ajili ya kufuatilia taarifa hizo ambapo iliweza kuungana na mwalimu mkuu wa shule ya msingi anayosoma ‘bi harusi’ huyo, Hamad Mnaguzi na viongozi wengine wa kamati ya shule akiwemo mwenyekiti wa serikali ya kijiji, Shaban Zageni.
Kijana aliyefahamika kwa jina la Andrew Vincent anayetuhumiwa kuoa mwanafunzi.
OFM na viongozi hao walikwenda nyumbani kwa wazazi wa mtoto aliyeozeshwa na kumkuta mama yake aliyejitambulisha kwa jina la mama Wastara huku akikataa kutaja alikokwenda baba wa mtoto huyo pamoja na wanandoa wenyewe.
OFM ilipomuhoji kama anatambua tukio la mtoto wake kuozeshwa alikataa kuwa, hana mtoto wa shule ambaye ameolewa hivi karibuni huku akidai kuwa yeye ana mtoto mmoja tu ambaye aliolewa miaka mitatu iliyopita.
Baada ya kubanwa, ndipo akakiri kumuozesha bintiye na kudai kuwa familia ilifanya hivyo kutokana na ugumu wa maisha.
Hata hivyo, mama huyo akasema hajui makazi ya mwanaume huyo yalipo.
OFM kwa kushirikiana na viongozi hao wa serikali walimchukua mama huyo hadi kwenye ofisi ya serikali ya mtaa huo na kumlazimisha aelekeze alipo mwanae ndipo mjomba wa Wastara alijitokeza na kusema anapajua walipo wanandoa hao.
Saa 3 usiku, OFM na viongozi hao walifika kwenye kituo cha mafuta kilichopo Msata, Bagamoyo, Pwani na katika uliziaulizia, nyumba hiyo ilipatikana ambapo bwana harusi na baba yake walikimbia.
OFM ilifanya jitihada za kumsaka kijana huyo na kufanikiwa kumnasa na kumhoji kwa kina sababu ya kuoa denti wa shule ya msingi ambaye walimu wake wanamtambua kuwa ni mwanafunzi wao, akajitetea kuwa, aliwasiliana na wazazi wa binti huyo baada ya kukutana naye njiani na kuvutiwa kumuoa.
Wastara akiwa na begi lake.
“Mimi sikujua kama mwanafunzi niliambiwa hasomi, najuta! Hapo nimetoa mahari shilingi 300,000 lakini sina budi kuachana naye,” alisema kijana huyo.
Akaendelea: “Nimelala naye siku moja tu baada ya ndoa, ni vyema wanirudishie mahari yangu.”
Kwa upande wake denti huyo alisema hakuwa tayari kuolewa mapema ila kwa kuwa alikuwa haendi shule akaona bora afanye hivyo.
Baada ya mahojiano hayo, OFM na viongozi hao walimwamuru binti arudi kwa wazazi wake ili kufanyiwa mpango wa kuendelea na masomo huku wanandoa hao wakiangua vilio kwa kuwa ndoa yao ilikuwa bado changa.

Post a Comment

 
Top