0


Moja kati ya maadui wakubwa wa usingizi ni mdudu ‘kunguni’ ambaye anaweza kumfanya mtu anayepanga kujipumzisha kuhisi anaadhibiwa kwa kufinywa.
 
Wanafunzi wa shule ya Sekondari ya Pugu iliyoko Dar es Salaam, ambayo ina historia ya pekee kwa kuwa ni moja kati ya shule alizofundisha muasisi wa Taifa hili, mwalimu Julius Kambarage Nyerere wamekumbwa na mtihani mkubwa na kulazimika kuyakimbia mabweni yao kutokana na kushambuliwa vikali na mdudu aina ya ‘kunguni’.
 
Kilio cha wanafunzi hao  wa shule hiyo ya bweni inayochukua wanafunzi wa kiume pekee kimeripotiwa na Edson Mkisi Jr, mtangazaji wa kipindi cha Hatua Tatu cha 100.5 Times Fm aliyetembelea shule hiyo.
 
Mkisi alipata nafasi ya kuongea na baadhi ya wanafunzi wa shule hiyo ambao walieleza hali ilivyo na kwamba kwa jinsi ambavyo wanaongezeka, imewabidi watumie muda mwingi kuwa madarasani hata nyakati za usiku na hata kulala huko.

Hali inayowafanya washindwe kupumzika vizuri na kuathirika kwa kiasi kikubwa kimasomo.
 
Nae Makamu Mkuu wa shule ya Pugu, amethibisha kuwepo kwa tatizo hilo na kwamba tayari uongozi wa shule hiyo umemuomba msaada meya wa Ilala, Jerry Slaa ili waweze kusaidiwa kuwatokomeza wadudu hao na ameahidi kuwasaidia.
 
Hata hivyo, wanafunzi hao wamekiri kuwa kumekuwepo na jitihada za kutosha zinazofanywa na wanafunzi na walimu katika kupambana na wadudu hao lakini wadudu hao hutoweka kwa muda na kurudi tena hasa kipindi cha joto.
 
Uamuazi wa wanafunzi hao kulala madarasani ni hatari zaidi kwa kuzingatia tishio la ugonjwa hatari wa Dengue unalolikabili jiji la Dar es Salaam, unaoambukizwa kwa kuumwa na mbu.
 
>>Times 100.5FM

Post a Comment

 
Top