0

Majaji Zanzibar wameondolewa ulinzi wa Jeshi la Polisi kwenye makazi yao na wengine kuanza kulindwa na walinzi wa kampuni binafsi, imebainika.

Uchunguzi wa gazeti la mwananchi umebaini kuwa, majaji hao wameondolewa ulinzi kwenye makazi yao takriban mwaka mmoja sasa hali inayowafanya kuishi kwa mashaka.
Akizungumza mjini hapa, Jaji Mkuu wa Zanzibar, Omar Othman Makungu alithibitisha kuwapo hali hiyo na kwamba mamlaka husika imeanza kufuatilia.
Jaji Makungu alisema waliwahi kujadili na kufikia hatua nzuri kwamba, vikosi maalumu vya SMZ ndiyo vifanye kazi hiyo.
Hata hivyo, alisema tatizo kubwa ni pale jaji anapokuwa na mke zaidi ya mmoja na kuishi sehemu tofauti.
Kwa upande wake, Kamishna wa Polisi Zanzibar, Hamdani Omar Makame alithibitisha askari wa Kikosi cha Kuzuia Ghasia(FFU) kuondolewa kwenye shughuli za ulinzi.
Kamisha Hamdan alisema walitoa mapendekezo serikalini kutaka kila nyumba ya jaji kujengwa kibanda maalumu kwa ajili ya walinzi, lakini jambo hilo halijafanyiwa kazi hadi sasa.
Wakizungumza kwa masharti ya kutotajwa majina yao, baadhi ya majaji walisema tatizo hilo ni la muda mrefu na hawaelewi sababu ni nini.

Source: Mwananchi

Post a Comment

 
Top