Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ametoa salamu za rambirambi na pole nyingi kwa Rais wa Jamhuri ya Nigeria Mheshimiwa Goodluck Jonathan na wananchi wa Nigeria kufuatia mfululizo wa vitendo vya ugaidi ambavyo vimepoteza maisha ya maelefu ya wananchi wa nchi hiyo na kutekwa nyara kwa mamia ya watu wakiwemo wanafunzi wa kike wa sekondari.
Katika
salamu zake za pole kwa Rais Jonathan, Rais Kikwete amesema: “Napenda
kutoa salamu za rambirambi na pole zetu nyingi kwako Mheshimiwa Rais na
wananchi wa Nigeria kufuatia mfululizo wa vitendo vya kigaidi ambavyo
vimepoteza maisha ya maelfu ya wananchi wa nchi hiyo na wengine kutekwa nyara.
Tumekuja kuonyesha mshikamano wetu na wananchi wa Nigeria.”
Rais
Kikwete ametoa pole hizo mwanzoni mwa hotuba yake kwenye mkutano wa marais
uliozungumzia umuhimu wa miundombinu ya kimkakati katika Afrika ikiwa ni sehemu
ya Kongamano la Uchumi Duniani (WEF) Afrika kwenye Hoteli ya Transcorp Hilton
mjini Abuja, Nigeria.
Akizungumza
mbele ya Rais Jonathan na viongozi wengine wa Afrika, Rais Kikwete amemwambia
kiongozi huyo wa Nigeria: “Tulishauriwa sana tusije kuhudhuria
kongamano hili kwa sababu ya hali ya usalama. Lakini tusingefika tungewapa
ushindi magaidi hawa ambao wanasumbua sehemu kubwa ya Bara letu. Mheshimiwa
Rais sala zetu ziko nawe na wananchi wa Nigeria katika kipindi hiki kigumu.”
Serikali
ya Nigeria imekuwa inapambana na vikundi vya kigaidi na hasa kile cha Boko
Haram ambacho kimekuwa kinaendesha kila aina ya ugaidi hasa katika maeneo ya
kaskazini ya nchi hiyo.
Wiki
tatu zilizopita, kikundi hicho ambacho lengo lake kuu ni kupinga elimu ya
magharibi kiliteka watoto zaidi ya 200 wa kike kutoka mabweni ya shule moja ya
sekondari kaskazini mwa nchi hiyo.
Mpaka
sasa watoto hao hawajapatikana, jambo ambalo linaipa shinikizo kubwa Serikali
ya Nigeria. Boko Haram kimetishia kuwauza sokoni watoto hao wa kike.
Siku
mbili zilizopta, kikundi hicho kiliteka nyara watu wengine wanane na usiku wa
jana, kimeua watu wanaokadiriwa kufikia 300 katika vijiji mbali mbali vya eneo
la kaskazini mwa nchi hiyo.
Imetolewa
na:
Kurugenzi ya
Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR
ES SALAAM.
8 Mei, 2014
Post a Comment