SPIKA wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Anne Makinda amesema ni marufuku kwa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kufanya shughuli zake ndani ya Bunge la Bajeti.
Alisema hayo juzi bungeni baada ya
Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni Freeman Mbowe kutangaza baraza
kivuli la mawaziri na kusema hicho ndiko kikosi cha ukawa ndani ya
Bunge.
Spika Makinda alimtaka Mbowe kuhakikisha
Ukawa inafanya kazi zake nje ya Bunge na si ndani ya Bunge kwani
wanapokuwa ndani ya Bunge wanakuwa ni kambi ya upinzani bungeni na si
vinginevyo.
“Ukawa ndani ya Bunge haipo, mnakumbuka shuka kumekucha, baraza lenu ni International Standard na miaka ya nyuma nilishawahi kuwashauri kitu kama hicho lakini mkakidharau na kuona hakina maana, nawapongeza sana, lakini mmekumbuka shuka kumekucha,” alisema.
Pia Spika Makinda alilitaka baraza hilo kivuli kutoa ushirikiano na wabunge wengine ili kufanya kazi ya kuendeleza watu.
“Watanzania hawajui nani anatoka wapi ila wanachotaka ni maendeleo yatakayosaidia kuboresha hali zao za maisha, wanataka kuona barabara nzuri na hata mazao yao yananunuliwa,” alisema.
Uteuzi huo ulihusisha vyama vya Chadema,
CUF na NCCR Mageuzi ambapo baraza hilo kivuli lina mawaziri 29 ambapo
watashika nafasi za uongozi katika kipindi kilichobaki kuelekea uchaguzi
mkuu mwakani.
Post a Comment