Vijana wasiopungua 45,000 watakaomaliza kidato cha sita watajiunga na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwa mujibu wa sheria na watakaokwepa mafunzo hayo ya miezi mitatu, watashtakiwa.
Mpango huo wa kupitisha JKT wahitimu wa kidato cha
sita na vyuo, ambao ulifutwa mwanzoni mwa miaka ya 90 kutokana na
matatizo ya kifedha na kurejeshwa bila mafanikio ya miaka ya hivi
karibuni, ulilenga kujenga uzalendo kwa vijana na kuongeza ukakamavu.
Jana Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga, Dk
Hussein Mwinyi alisema utaratibu huo ni wa kisheria na si hiari, hivyo
wahitimu wa kidato cha sita watambue kuwa ni kosa kukaidi wito wa
kujiunga na JKT.
Dk Mwinyi, aliyekuwa anawasilisha bungeni
makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake, alisema katika mwaka wa
fedha 2014/2015, vijana watakaojiunga na jeshi watafanya hivyo kwa awamu
tatu.
Alisema awamu ya kwanza itahusisha vijana 20,000
ambao wataingia katika mafunzo hayo Juni hadi Septemba 2014 na kufuatiwa
na wa awamu ya pili itakayochukua vijana 14,450 kuanzia Oktoba hadi
Januari 2015 wakati awamu ya tatu ya vijana 10,550 itaanza Januari hadi
Aprili 2015.
Hata hivyo, kumekuwepo na mwingiliano wa muda wa
kujiunga na jeshi hilo na wa kujiunga na masomo ya juu. Kati ya vijana
15,000 waliotakiwa kujiunga na jeshi hilo kati ya Oktoba 2013 na Januari
2014, waliojiunga walikuwa 1,002 tu.
Alipoulizwa kuhusu mwingiliano huo, naibu waziri
wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Jenister Mhagama alisema atatoa ufafanuzi
huo leo.
Akichangia mjadala wa bajeti hiyo, mbunge wa viti
maalumu (CCM), Esther Bulaya alitaka mafunzo ya JKT kwa wabunge
yafanyike kwa miezi miwili hadi mitatu badala ya wiki mbili.
Bulaya, ambaye alipitia mafunzo hayo pamoja na
wabunge wenzake wakati mpango huo uliporejeshwa mapema mwaka jana,
alisema kuwa hali hiyo itawafanya wabunge hao kujifunza mambo mengi
zaidi.
Bulaya aliwataja baadhi ya wabunge vijana
wanaotakiwa kujiunga na mafunzo hayo kuwa ni John Mnyika
(Chadema-Ubungo) na Catherine Magige (viti maalumu-CCM).
“Mheshimiwa Spika naomba uwaruhusu wabunge kwenda kwenye mafunzo kwa miezi miwili hadi mitatu,” alisema na Bulaya na kuongeza:
“Katika kambi za JKT kuna tatizo la vifaa vya
afya, hivyo wizara iliangalie hilo ili wanaokwenda katika mafunzo hayo
wapate tiba sahihi na kwa wakati.”
Wataka muda uongezwe
Akiwasilisha maoni ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya
Ulinzi na Usalama kuhusu wizara hiyo, mjumbe wa kamati hiyo, Vita
Kawawa alipendekeza muda wa JKT uongezwe hadi miezi sita.
Kawawa alisema ingawa Serikali inasema kuongeza
muda huo kunashindikana kutokana na mabadiliko ya mihula ya masomo
vyuoni, bado wanasisitiza umuhimu wa kuongeza muda wa mafunzo.
/span>
/span>
Kamati hiyo imeshauri vijana wote wanaomaliza
kidato cha sita kujiunga na JKT na wale ambao hawataripoti kwa mafunzo
bila sababu za msingi, Serikali iwachukulie hatua za kisheria.
Bajeti ya Wizara
Kuhusu bajeti, Dk Mwinyi alisema wizara yake
itatumia Sh1.26 trilioni kwa mwaka ujao wa fedha kwa ajili ya kutekeleza
shughuli mbalimbali, zikiwamo kununua ndege za kivita.
Dk Mwinyi aliliambia bunge kuwa kati ya Sh1.26
trilioni, Sh1.0 trilioni zitatumika kwa ajili ya matumizi ya kawaida,
wakati kiasi cha Sh249 bilioni zitatumika kwa ajili ya matumizi ya
maendeleo.
Kwa mujibu wa Dk Mwinyi, miongoni mwa shughuli
zitakazotekelezwa na wizara hiyo ni pamoja na kununua vifaa na zana za
kijeshi, ikiwamo vifaa vya uhandisi wa medani na ndege za kivita.
Pia,alisema wizara itaanza ujenzi wa gati katika
Kamandi ya Jeshi la Wanamaji Kigamboni, kuboresha mifumo ya mawasiliano
ya ndani na nje ya vikosi vya kambi za jeshi na kuendelea na ujenzi wa
nyumba 6,064 za makazi ya wanajeshi.
Dk Mwinyi alizitaja shughuli nyingine
zitakazofanywa kuwa ni kukamilisha ujenzi wa shule ya mafunzo ya awali
ya kijeshi (RTS), eneo la Kihangaiko, Pwani na Chuo cha Ukamanda na
Unadhimu (CSC), Tengeru Arusha.
Pia,wizara itaanza ujenzi wa hospitali kuu ya
jeshi eneo la Mataya mkoani Pwani, kuimarisha ushirikiano na nchi
nyingine duniani katika nyanja za kijeshi na pia kulipa madeni ya
kimkataba.
Hata hivyo, Dk Mwinyi alisema kuwa pamoja na bunge
kuidhinishia wizara hiyo Sh1.1 trilioni kwa mwaka unaoishia Juni 30
mwaka huu, hadi Machi ilikuwa imepokea Sh768.4 bilioni, sawa na asilimia
69.7.
>>Mwananchi
>>Mwananchi
Post a Comment