0


Katibu wa Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye amepeleKa ‘msiba’ Chadema, baada ya kusomba wanachama wa chama hicho wanaosoma katika Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (Saut), tawi la Mwanza, wakiongozwa na Rais wa Serikali ya Wanafunzi (Sautso), Philbert Saimon.
 
Wanachama hao wa Chadema waliamua kuhama chama hicho jana, katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa Shule ya Msingi Nyamalango, nje kidogo ya Chuo cha Saut, ambapo Nape alikuwa mgeni rasmi.
 
Akieleza sababu zilizomfanya ahame Chadema, Saimon  alisema: "Tumepoteza muda mrefu kuwatumikia watu wasio na mwelekeo, watu ambao wamejaa uongo na ubabaishaji mwingi, wakati sie tunahangaika, tunaacha masomo kwa ajili yao, watoto wao wanasoma vizuri, tumechoka kutumiwa, CCM ndio mpango mzima.”
 
Vijana wengine walipohojiwa kwa nyakati tofauti walisema kwa muda sasa CCM imeanza kwa kasi kubwa kurekebisha upungufu uliokuwa ukikikabili chama hicho na hivyo kuvutia wengi .
 
Naye Nape aliamua ‘kufuta nyayo’ za viongozi wa wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, waliojiundia kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi  (Ukawa), kwa kujibu hoja zilizoibuliwa na Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa na msemaji wa Ukawa, Tundu Lissu.
 
Nape alisema: "Wenzangu walikuja hapa na talalila nyingi sana, leo nitajibu hoja moja baada ya nyingine na nitaanza na la changamoto za elimu."
 
Alisema mchakato wa ujenzi wa shule za sekondari za kata ulipoanza, wapinzani wengi walikejeli na kuzipa majina mbalimbali, lakini walioanza shule za sekondari za kata mwaka ule leo ndio wanamaliza vyuo vikuu nchini na wengine wako nje ya nchi.
 
Alieleza jinsi Serikali kwa kushirikiana na wananchi, inavyojenga maabara kwenye sekondari za kata na kupeleka walimu kwa mamia kila wilaya, ili kuboresha elimu nchini na kuwataka wananchi kupuuza wote wanabeza mafanikio hayo.
 
Kuhusu Ukawa, Nape aliendelea kusisitiza msimamo wa CCM wa kutowabembeleza wajumbe hao kurudi katika Bunge Maalumu la Katiba, akidai ni kupoteza muda kwa watu wasiokuwa na nia njema ya kuhakikisha Katiba mpya inapatikana.
 
"Hawa wenzetu wamegeuza huu sasa mchezo kila wakigoma wanabembelezwa, wanapewa juisi Ikulu wanarudi bungeni, sasa wamegeuza mchezo, safari hii habembelezwi mtu, kama noma na iwe noma.
 
"Sheria ya mchakato Katiba mpya wameshiriki tukatunga wote, na sheria imeeleza wazi kuwa tutakuwa na awamu tatu kuu za kukamilisha mchakato wa Katiba mpya nchini.
 
“Awamu ya kwanza ni ya kukusanya maoni, awamu ya pili ni ya kujadili na kuyachambua maoni na awamu ya tatu ni ya kuipitisha kwa kupiga kura za maoni kwa wananchi. Asiyetaka kufuata utaratibu tuliojiwekea, hana nia njema na upatikanaji wa Katiba mpya,” alisema Nape.
 
Nape alisisitiza kuwa hoja ya kuwa CCM haitaki Katiba mpya ni hoja mfu kwani aliyetangaza na kuanzisha mchakato ni Mwenyekiti wa Taifa wa CCM na Serikali ndiyo inayotoa fedha za kugharamia mchakato huo na  kama CCM isingetaka Katiba mpya, isingefanya hayo yote.
 
"Hata mjadala wenyewe na utoaji wa maoni kwenye rasimu hakuna taasisi iliuchukulia kwa umuhimu mkubwa mchakato huo kuliko CCM, mpaka tumetoa maoni yetu kwa maandishi na machapisho kadhaa.
 
“Sasa wenzetu wanaounda genge la Ukawa wakati hata mmoja wao hana chapisho lolote zaidi ya ubabaishaji na kelele. Ndio maana wanafikia mahali wanadai muundo wa serikali tatu utadhibiti ufisadi nchini, nataka kujua serikali tatu inadhibiti vipi ufisadi? Si lazima kuwa na serikali tatu ndio udhibiti ufisadi," alisema Nape.
 
Nape alisisitiza kuwa Ukawa itasambaratika bila mkono wa CCM, na kuwa CCM hawana muda wa kuhangaika kusambaratisha upinzani kwani upinzani utajisambaratisha wenyewe kwa mbegu mbaya wanayopanda.
 
"Huwezi kupanda mahindi ukavuna uwele, kile unachopanda ndicho utakachovuna," alisema.

Post a Comment

 
Top