Huu ni mchezo ambao mashabiki wa soka wanausubiri kwa hamu kubwa wakiamini pia utatumika kutoa majibu halisi ya fainali hizo zinazofanyika nchini Brazil.
England na Italia ni nchi ambazo ligi zake ni maarufu sana, huku zikiwa zinafuatiliwa kwa karibu sana na mashabiki wa soka duniani kote.
Ukitaja kwa upande wa Tanzania, Ligi Kuu ya England, maarufu kama Premier League, yenye timu kubwa kama Liverpool, Manchester United, Arsenal na Chelsea, watakuambia ndiyo ligi bora zaidi kutokana na kufuatiliwa kwa karibu zaidi na mashabiki wa hapa nchini.
Lakini ukiitaja Serie A, ambayo ina timu kubwa kama Juventus, Inter Milan na AC Milan, utaelezwa kuwa hii ni ligi bora.
Lakini Italia asimilia kubwa ya wachezaji mahiri wanaichezea timu yao ya taifa, kitu ambacho kitaonyesha tofauti kubwa ya mchezo huo wa leo usiku utakaopigwa katika Uwanja wa Arena Amazonia, Manaus.
Ushindi kwa timu yoyote au sare kwenye mchezo huu zitatoa picha halisi juu ya kundi D, ambalo limekuwa likitajwa kama kundi la kifo likiwa lina timu pia za Uruguay na Costa Rica.
Kila timu itakuwa inacheza kwa tahadhari kubwa kwa kuwa inafahamu matokeo mabovu kwenye mchezo huu yanaweza kuwa sababu pekee ya kuondoka kwenye fainali hizo na kurejea nyumbani kuanzia kwenye hatua ya makundi tu.
Lakini hazitakuwa na haja ya kutumia nguvu kubwa sana kwa kuwa ni hivi karibuni tu zilikutana kwenye michuano ya Kombe la Euro na England kuondolewa kwa mikwaju ya penalti.
Mchezo wa leo labda unaweza kuwa sawa na ule wa Kombe la Euro ambao Andres Pirlo aliibuka staa kwa kumiliki sehemu kubwa ya mchezo, lakini pia alifunga penalti safi ambayo iliwamaliza kabisa England.
Katika mchezo wa leo, England wataanza kwa kasi kubwa huku wakiwatumia wachezaji wake wa pembeni kukimbia, ambao ni Sterling, Barkley na Sturridge, kwa ajili ya kuichanganya ngome ya Italia.
Lakini ni timu ambayo haitakiwi kufanya kosa kubwa kwenye safu yake ya ulinzi kwa kuwa wachezaji wake wengi wa nyuma wanaonekana kutokuwa imara sana na kutokuwa na uzoefu wa kutosha.
Gary Cahill, Cris Smalling, Glen Johnson na Leighton Baines, siyo safu ambayo ina uzoefu wa kutosha, lakini inaweza kufanya maajabu.
Safu ya kiungo katikati ambayo itakuwa ikiongozwa na Frank Lampard na Steven Gerrard, haionekani kuwa na tatizo kubwa sana kwa kuwa mastaa hawa wana uzoefu wa kutosha na huu hautakuwa mchezo wao wa kwanza kucheza dhidi ya Italia.
Lakini pia watakuwa hawana hofu kubwa kwenye safu yao ya ushambuliaji kwa kuwa mchezaji wao tegemeo, Wayne Rooney, ameshaeleza kuwa hizi ni fainali zake za kipekee ambazo anatakiwa kufanya vizuri baada ya kushindwa kufurukuta mara mbili huko nyuma, inaaminika kuwa anaweza kusaidiana vyema na Danny Welbeck.
Kumekuwa na maswali mengi juu ya uwezo wa mshambuliaji huyo wa Manchester United, lakini inaaminika kama Italia watafanya makosa basi anaweza kuwa na madhara makubwa kwao.
Upande wa Italia wenyewe hali ni tofauti kwani ni kikosi ambacho kimejaa wachezaji wengi sana wenye uzoefu na michuano ya kimataifa.
Kocha wa timu hiyo, Cesare Prandelli, alitangaza kikosi cha wachezaji 23, huku asilimia kubwa wakiwa na uzoefu mkubwa kuanzia kipa wa timu hiyo, Gianluigi Buffon, anayekichezea kikosi cha Juventus.
Wakati England wenyewe wachezaji wake wote waliopo kwenye kikosi wanacheza soka lao nyumbani, kwa upande wa Italia wao wana wachezaji watatu; Salvatore Sirigu, Thiago Motta na Marco Verratti ambao wanacheza nje ya nchi hiyo wakiwa wameitwa kutoka kwenye kikosi cha PSG.
Kipa Buffon ambaye pia alicheza kwenye fainali zilizopita, anapewa nafasi kubwa ya kuanza kwenye lango la Italia akiwa ana uzoefu wa kutosha.
Kwake atakuwa anafanana kidogo na kipa wa England, Joe Hart, kwa kuwa wote wamefanikiwa kutwaa ubingwa wa nchi yao msimu uliopita, lakini kwa uzoefu bado kipa huyo mwenye umri wa miaka 36 anaonekana kuwa juu zaidi.
Kwa upande wa safu ya ulinzi, bado Italia wanaonekana watakuwa na wachezaji wengi wazoefu kama Ignazio Abate, Andrea, Leonardo Bonucci, Giorgio Chiellini na Gabriel Paletta.
Lakini England wanaweza kuisumbua safu yao ya kiungo kama watakubali kucheza kwa kasi kwani itakuwa na wachezaji wazoefu pia kama Alberto Aquilani, Antonio Candreva, Daniele De Rossi, Claudio Marchisio na Andrea Pirlo ambao kasi yao siyo ya juu sana.
Wakimtegemea zaidi mshambuliaji wao Ciro Immobile na Antonio Cassano ambao wameonekana kuwa kwenye kiwango kizuri kwenye Ligi Kuu ya Italia msimu uliopita, Italia hawatakiwi kufanya kosa lolote.
“England wana wachezaji wengi vijana ambao ni hatari sana kama utawaacha wakakaa na mpira kwa muda mrefu, hakika tunataka kushinda mchezo huu na kama ni hivyo basi lazima tuzuie kasi yao.
“Najua wana wachezaji wazuri kama Frank Lampard, Oxlade Chamberlain, Rooney na Sturridge na kipa wao Joe Hart, hivyo kama tunataka ushindi ni lazima tujitume sana,” alisema kocha wa Italia, Cesare Prandelli
Post a Comment