Lakini kuna mambo mengi ya kufanya ili uweze kujisogeza kuwa mke wa mtu hapo baadaye, kama wewe ni mfuatiliaji mzuri wa kona hii, naamini ukiyafanyia kazi ninayoandika, yatakupa mwanga na kuwa mke bora siku za usoni. Wapo walilamika kuwa wanabezwa kwa kufikisha umri wa miaka 35 na zaidi bila kupata mwanaume ambaye anataka kumuoa, wengine wakasema wanaitwa wana nuksi, balaa na mikosi na kwamba wasitarajie kabisa kuolewa tena!

Siyo kweli, achana na mawazo haya ya kukatisha tamaa, futa maapizo haya ya kusinyaisha moyo, amini unayo nafasi kubwa sana ya kuwa mke mwema baadaye. Yote yanawezekana rafiki zangu. Tulia, kuwa makini, omba kwa Mungu, halafu vuta subira, atakuja mwenyewe!
Usitumie udhaifu huo kubadilisha wanawame kila siku ukisubiri bahati, dada yangu, ndoa si bahati, mume hatafutwi ANAKUJA MWENYEWE muda ukifika. Sina shaka kuna kitu kinaanza kuingia kichwani mwako....eenheee....okey!

Siku zote jitahidi kuwa bora katika sehemu katika maisha yako ili uonekane muungwana na kujingenezea historia nzuri. Ukiwa muungwana, utaaminiwa, utapendwa na utaheshimika pia, zaidi ya yote utakubalika na kila mtu, kukubalika na kila mtu ni mwanzo mzuri wa wewe kukubalika na mwezi wako wa milele.
Imekuwa kawaida wanaume kuamua kuwatoa ‘out’ wapenzi wao, wakati mwingine huamua kutoka na wanawake ambao wanatarajia kuwa nao hapo baadaye. Hapa nazungumzia juu ya wale ambao wamekuwa katika urafiki katika muda mrefu lakini lengo la jamaa ni kumpima ili baadaye aweze kuwa mwenzi wake.

Tatizo sugu katika hii mitoko ni baadhi ya wanawake kwenda na ‘kampani’ yao/zao. Utakuta mtu kapewa mwaliko, anaamua kubebana na mashoga zake watatu au wanne, eti wanamsindikiza! Hata kama ni mmoja, kwani uliambiwa uende na mtu? Sasa soma mtiririko ufuatao, ujifunze kitu kama una tabia hiyo au ulikuwa na mpango wa kufanya hivyo.

INAKUPUNGUZIA SIFA
Kama ulikuwa ni mpenzi wa jamaa huyo, hapa utakuwa umeshapunguza credit za kuwa mke. Kwa vyovyote vile, hata kama hatakuambia, atabaki na donge moyoni. Atakuwa na maswali mengi sana, lakini hatakuwa na majibu na muda wote atakuwa amejenga tabasamu la kutengeneza.
Amka. Kama una tabia hii na una mpango na mshkaji acha, other ways uwe na nia ya kumchuna na kuanza zako, lakini kama unataka kuingia kwenye ndoa, utampoteza!

ATAJUA UNAMCHUNA!
Maswali kichwani mwake yatakuwa mlima, lakini kubwa litakalotawala ni ile hali ya kuhisi kabisa kwamba unafanya buzi. Yes...unamfanya buzi, kwasababu kama ni kinyume chake, kwanini uongozane na kampani? Kama alikuwa na nia wewe, haraka atageuka, ana haja gani ya kuwa na mwanamke mfujaji wa fedha?

UTAMWOGOPESHA...
Kama ndiyo anakutaka na wewe kwa mara ya kwanza, utamwogopesha kuongea chochote. Kwanza atajua umekuja na watu ili asiweze kuongea, lakini pia ataogopa kukualika katika mtoko mwingine, maana utakuwa umejipotezea sifa ya ustaarabu.

BAJETI YAKE VIPI?
Vyovyote itavyokuwa, utakuwa hujui ana bajeti kiasi kwa ajili ya siku hiyo, lakini kubwa zaidi hufahamu ana kiasi gani kwenye pochi yake siku hiyo. Hata kama ungekuwa wewe, kwa hakika usingeona bajeti yako ikiharibiwa bila mpangilio.
Halafu utafiti usio rasmi unaonyesha kwamba, marafiki wanaobebwa katika mitoko isiyo yao, huwa wanakula na kunywa vinywaji vya bei ghali zaidi hata mualikwa. Hili ni tatizo, kama hana pesa za kutosha na network ya ATM haisomi itakuwaje?

UNAWEZA KUUMBUKA
Iwe unamkomoa, hujui au ni bahati mbaya, lakini vipi kama utakutana na mwanaume ‘fyatu’ kidogo, ambaye hajali. Unajua kitakachotokea, anaweza akalipa bili yako na yake, halafu akasema hao wengine hawakuwa kwenye bajeti yake, kwa maana hiyo ulipe wewe au wajilipie wenyewe! Aibu kiasi gani?
Mkatili zaidi, anaweza akawaacha mkaagiza sana, bili ikishakuwa kubwa anaenda kaunta na kulipa vyake tu, halafu anamwagiza aje awadai. Akija kwenu anajifanya anakwenda msalani, kumbe kawaachia msala, itakuwaje? Ukute na wewe kwenye pochi yako una elfu kumi tu, halafu bili 45,700, utaumbuka!

UMENIPATA?
Umeona eeh! Nadhani ni vizuri kama una haka katabia ukabadilika, kwani si njema hasa kwa mwanaume ambaye unatarajia awe wako. Ukipewa ofa ya mtoko, nenda peke yako.
Ukweli ni kwamba, ukibebana na wenzako unaibua hisia tofauti ambayo inaweza kukupotezea pointi za kuwa mwenzi mwema hapo baadaye. Umenisoma? Ok! Ahsateni sana kwa kukubali kubadilika.

Elimu inayotolewa na kona hii ni fundisho kwa wengi walio katika uhusiano. Nashukuru sana kwa wale wanaowasiliana nami na kunipongeza huku wengine wakitoa maoni yao na wale wanaoomba ushauri. Hiyo ni alama tosha kwamba wengi mnajifunza kupitia hapa Uwanja wa Huba, karibuni tena!

Mada ya wiki jana ilikuwa na changamoto sana, ilipokelewa vyema na wasomaji wengi, hasa walionipigia na kutaka ufafanuzi zaidi; Labda niendelee kusisitiza kwamba, suala la kuolewa au kutokuolewa halihusiani kabisa na nuksi na uzuri wa sura!
 
Top