Mhitimu bora wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 2014, Doreen Kabuche (22), aliushangaza umma uliohudhuria maafali ya 44 ya chuo hicho baada ya kutangazwa kuwa kinara kwa ufaulu kwa kupata alama A 32 na B+ sita kati ya masomo 38 ya shahada ya Takwimu Bima (Actuarial Science).
Kwa
alama hizo, Doreen alipata wastani wa alama za ufaulu (GPA) 4.8 na
kuacha alama ya 0.2 ili kufikia kiwango cha juu kabisa cha ufaulu cha
alama tano, hivyo kupata shahada ya kwanza daraja la kwanza.
Akizungumza na NIPASHE katika mahojiano maalum mwishoni mwa wiki, Doreen anayeishi Kigogo Mwisho, jijini Dar es Salaam alihitimu shahada hiyo akiwa miongoni mwa wanafunzi 28 wa darasa lake, lakini akihitimu sambamba na wanafunzi wengine 5,745, wanawake wakiwa ni 2,298 wa shahada ya kwanza.
Akizungumza na NIPASHE katika mahojiano maalum mwishoni mwa wiki, Doreen anayeishi Kigogo Mwisho, jijini Dar es Salaam alihitimu shahada hiyo akiwa miongoni mwa wanafunzi 28 wa darasa lake, lakini akihitimu sambamba na wanafunzi wengine 5,745, wanawake wakiwa ni 2,298 wa shahada ya kwanza.
Shahada
hiyo inayotolewa katika Shule ya Sayansi ya Asili (CoNaS) chuoni hapo,
ni miongoni mwa taaluma adimu nchini. Ilianza kufundishwa chuoni hapo
mwaka 2011.
Miongoni
mwa taasisi ambazo zitafurahia taaluma hiyo kuanza kupata wataalam
nchini ni pamoja na mifuko ya hifadhi ya jamii ambayo hulipa fedha
nyingi kupata huduma hiyo kwa wataalam kutoka nje ya nchi na kwa gharama
kubwa.
Alipopewa
nafasi ya kuzungumza mbele ya mamia ya wanafunzi wenzake na wageni
waalikwa kwenye ukumbi wa Mlimani City, aliishia kutoa shukrani kwa
wahadhiri, wanafunzi wenzake na wote waliomsaidia katika mafanikio yake
kitaaluma.
Ili
kupata wastani wa ufaulu wa daraja la kwanza kwa kiwango cha GPA ya
4.8, mhitimu hulazimika kufaulu kwa kiwango cha juu kwa miaka yote ya
kuwa chuoni. Doreen alifanikiwa kutimiza sharti hilo baada ya kufaulu
masomo 32 kwa kiwango cha ‘A’ na masomo mengine sita kufaulu kwa alama
za B+ kati ya masomo yote 38 ya shahada yake; baadhi ya yale
yaliyomkwamisha kupata A yakiwa ni ‘Actuarial Mathematics’ na ‘Legal
Matters in Actuarial Industry’.
Mgawanyo
wa ufaulu wake kwa mwaka wa kwanza ulikuwa ni A za masomo 12 na B+ za
masomo mawili kati ya masomo 14; mwaka wa pili alifaulu kwa kupata A
katika masomo 10 na B+ mbili kati ya masomo 12 na mwaka wa tatu alifaulu
pia kwa kiwango cha alama A katika masomo 10 na masomo mengine mawili
akapata B+ kati ya masomo 12.
ALIKOTOKA
Tofauti
na fikra za wengi kuwa siku hizi wanafunzi bora hutoka katika shule
zinazotoza ada kubwa na kutumia Kiingereza kama lugha kuu ya
mawasiliano, maarufu kama English medium’, Doreen anathibitisha kuwa
hilo halina ukweli.
Katika
mahojiano na NIPASHE, alisema kuwa hajawahi kusoma katika shule hizo
zinazotoza ada kubwa za mamilioni ya fedha na badala yake, alipitia
katika shule za serikali kuanzia shule ya msingi mwaka 2004 hadi kidato
cha sita mwaka 2011.
“Shule
nilizosoma kabla ya chuo kikuu ni Mlimani (Shule ya Msingi) iliyopo
Chuo Kikuu Dar es Salaam sehemu ya Mlimani, kidato cha kwanza hadi cha
nne nilimaliza katika sekondari ya Forodhani na kidato cha tano na sita
katika shule ya sekondari Benjamin Mkapa. Kote huko usafiri wangu siku
zote ni wa daladala.
“Na
kama unavyojua, ni kugombana na makondakta kila asubuhi wakati wa
kupanda mabasi (daladala) kwenda shule na jioni wakati wa kurudi. Ila
yote hayo tumeyazoea na hivyo adha za usafiri hazikuwa tatizo kubwa,”
alisema Doreen na kuongeza:
“Juhudi,
kujiamini na kuzingatia maelekezo ya walimu ni muhimu. Aina ya shule ni
nyongeza tu kwa sababu siyo wote wanaosoma shule hizo za kitajiri
wamekuwa wakifaulu. Wapo wanaofanya vizuri, na wapo wanaofeli pia... ni
kama ilivyo kwenye hizi shule zetu (shule za serikali).”
KINARA KIDATO CHA SITA
Mafanikio
ya sasa ya Doreen hayakuja kwa bahati mbaya. Historia yake inaonyesha
kuwa kila hatua aliyopita alikuwa akifanya vizuri. Katika matokeo yake
ya kidato cha nne mwaka 2008, Doreen alifaulu kwa kiwango cha daraja la
kwanza akipata pointi tisa na kuchaguliwa kuendelea kidato cha tano
katika Shule ya Sekondari Benjamin William Mkapa baada ya kuchagua
mchepuo wa Uchumi, Hisabati na Jiografia (EGM).
Doreen
aliendeleza makali yake katika mitihani yake ya kidato cha sita baada
ya kufaulu kwa kiwango cha daraja la kwanza kwa pointi nne na kuwa
kinara wa mchepuo wa EGM Tanzania.
Kwa
matokeo hayo, akapata nafasi ya kuwa miongoni mwa wanafunzi bora
Tanzania walioitwa bungeni mwaka 2011 na kutambulishwa na Waziri Mkuu,
Mizengo Pinda, mbele ya wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na
kushangiliwa na wote waliokuwamo ukumbini.
“Hapo
shauku yangu ya kutaka kuongeza juhudi zaidi na kufanikiwa kama akina
Migiro (Asha-Rose), akina Tibaijuka (Profesa Anna) na akina Spika Anne
Makinda ikaongezeka. Nikapania kufanya vizuri hadi chuoni na sasa
namshukuru Mungu kuwa hatua hiyo pia nimeivuka salama na kufanikiwa,”
alisema Doreen.
Pamoja
na mafanikio yake kuanzia kidato cha kwanza hadi cha sita, Doreen
alisema kuwa hajawahi kujihusisha sana na masomo ya ziada maarufu kwa
jina la tuition na badala yake, alitumia muda mwingi kujisomea,
kujadiliana na wanafunzi wenzake na mara kadhaa kusaidiwa masomo
nyumbani na mjomba wake Charles Mayalla wa Taasisi ya Teknolojia Dar es
Salaam (DIT).
Doreen
alitangazwa kuongoza kwa ufaulu Chuo Kikuu Dar es Salaam ikiwa ni siku
chache tu baada ya msichana mwingine aitwaye Rachel Kiunsi wa Shule ya
Msingi Kimara 'B' jijini Dar es Salaam kuwa kinara wa somo la Hisabati
Tanzania baada ya kupata alama zote za somo hilo katika mithani ya taifa
ya darasa la saba.
MATARAJIO
Baada
ya kumaliza shahada ya kwanza, matarajio ya sasa ya Doreen ni kuendelea
na masomo ya shahada ya uzamili (masters) ambayo hata hivyo, anasema
mchakato wake (kwa masomo ya Actuarial Science) ni ghali kwani kabla ya
kujiunga anatakiwa kufanya mitihani kadhaa kabla ya kuanza shahada hiyo.
“Gharama
za mithani hii ni kubwa. Kuna mitihani ya hatua nyingi hadi kupata
nafasi ya kuanza kusomea masters na gharama zake kwa ujumla hufikia hadi
Sh. milioni 10. Hizi ni gharama kubwa. Ila kwa sasa sijakaa bure.
Wazazi
wangu bado wananiunga mkono na mwenyewe pia nimejifunza kuwa mpambanaji
tangu wakati nikigombana na makonda ili kupanda daladala na kuwahi
shule,” alisema Doreen.
“Na
hata sasa nimeshaanza mapambano ili kujiendeleza zaidi. Nimepata kazi
na fedha ninazopata nitaendelea kuzidunduliza kila mwezi ili nitimize
ndoto zangu. Hata kama nitalazimika kusubiri kwa mwaka na zaidi,
nitasubiri na mwishowe naamini kuwa Mungu ataniwezesha na kufanikisha
malengo,” alisema Doreen.
“Najua
hata hawa kina (Prof.) Tibaijuka, Migiro na wengine hawakufika walipo
sasa kirahisi. Walipambana, na mimi pia ninapambana ili siku moja
kufikia level zao,” alisema Doreen.
WAZAZI, FAMILIA
Akiwaelezea
wazazi wake, Doreen alisema kuwa baba yake (Kabuche) aliwahi kuwa
mfanyakazi wa benki kabla ya kuacha na kuwa mjasiriamali ambaye hivi
sasa yuko Mtwara. Mama yake aitwaye Janeth Kabuche pia ni mjasiriamali.
Doreen
alisema anawashukuru sana wazazi wake kwani mara zote wamekuwa
wakimsaidia kwa kila hali ili kutimiza malengo yake katika elimu.
Alisimulia kuwa hata alipotia fora kwa kutwaa zawadi za masomo yote
wakati wa mahafali ya kidato cha sita shuleni kwao Benjamin Mkapa mwaka
2011, wazazi wake walimtia moyo kwa kumnunulia kompyuta mpakato (laptop)
aina ya Dell.
“Kwetu
nimezaliwa peke yangu. Nikishatulia na kuanza maisha yangu binafsi
baada ya kumaliza mambo ya masomo nitapenda kuwa na watoto wengi ili
kuongeza ukubwa wa familia... walau wafikie watoto saba hivi.”
DINI, MUZIKI, FILAMU
Licha ya kufanya vizuri katika masomo, Doreen huwa haachi kujihusisha na masuala mengine ya kijamii.
“Kila
Jumapili huwa sikosi kwenda kwenye ibada katika kanisa letu la Kigogo
Luhanga. Vilevile mimi ni mpenzi wa muziki kama wa bendi ya Wazee wa
Ngwasuma (FM Academia), bongofleva na filamu pia huwa ninazitama...
(filamu) ninayoipenda inaitwa Think Like a Man, Act Like a Woman,”
alisema Doreen.
RATIBA AKIWA CHUONI
Doreen
alisema kuwa wakati wote akiwa chuoni alizingatia ratiba kuu
aliyojiwekea kila uchao, ambayo ni kwenda darasani bila kukosa kipindi
chochote na baada ya hapo alikuwa hakosi majadiliano na wanafunzi
wenzake kama Catherine John na Shamim Nuah.
“Sikuwahi
ku-dodge (kukacha) kipindi, sikuwahi pia kukosa discussion na wenzangu
bila sababu ya maana. Na siku moja moja za mwisho wa wiki tulikuwa
tukienda ku-refresh mind na wenzangu, hasa maeneo ya viwanja vya Sinza
na siku nyingine Mlimani City. Ila kila Jumapili ni lazima kwenda
kanisani pale chuo au kanisa la nyumbani kwetu Kigogo Luhanga,” alisema
Doreen.
Doreen
ana ndoto za akufuata nyayo za kina Prof. Anna Tibaijuka, Dk.
Asha-Rose Migiro na Anne Makinda kwa kuwa ni miongoni mwa wanawake
waliofanikiwa katika medani za taaluma, uongozi na siasa.
“Wapo
kina mama wengi wananivutia kwa rekodi zao kitaaluma na uongozi.
Tibaijuka na Migiro ni mfano mmojawapo. Naamini nikiongeza juhudi zaidi
nitakuwa kama wao... na hapo nitakuwa na nafasi ya kuboresha maisha
yangu, ya familia yangu na pia kuchangia maendeleo ya taifa langu. Na
hilo ndilo ninalowazia,” alisema.
Profesa
Tibaijuka ni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk. Migiro
ni Waziri wa Sheria na Katiba wakati Makinda ni Spika wa Bunge la
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
CHANZO: NIPASHE
Post a Comment