0
Nianze kwa kumshukuru Maulana kwa kutuwezesha kuiona salama siku ya leo, ni matumaini yangu kwamba msomaji wangu uko vizuri na unaendelea kulisongesha mbele gurudumu la maendeleo. Wiki iliyopita tulianza kujadili mada juu ya umuhimu wa kutoka ‘out’ na umpendaye. Tuliona jinsi kutoana out kunavyoweza kufufua mapenzi kati ya wawili wapendao bila kujali wameishi kwa muda gani katika uhusiano wa kimapenzi.
Tuendelee na sehemu ya pili ya mada yetu ambapo tutazungumzia mambo ya muhimu ya kuzingatia mnapotoka ‘out’ na yale ambayo hutakiwi kabisa kuyafanya unapotoka na umpendaye.
1. MAANDALIZI
Unapopanga kutoka na umpendaye, ni vizuri kufanya maandalizi ya kutosha ya vitu vyote muhimu ili siku ikifika, isionekane umekurupuka. Ni vizuri kufanya maandalizi ya sehemu unayotaka kumpeleka mwenzi wako na kuhakikisha ina utulivu wa kutosha na usalama.
Baada ya kuwa na uhakika na sehemu mtakayoenda, ni vizuri kujiandaa wewe binafsi. Andaa nguo safi, fanya usafi wa mwili ikiwa ni pamoja na kuoga vizuri na kupiga mswaki kwani mkiwa out, lazima mtasogeleana na mwenzi wako hivyo kama unanuka mdomo au jasho, unaweza kuwa kikwazo kwa mwenzi wako.
Hata kama hatakwambia, hatafurahia kuwa na wewe karibu. Unaweza pia kujipulizia marashi mazuri yatakayoongeza bashasha.

 
2. MPE KIPAUMBELE
Baada ya maandalizi ya awali kuwa yamekamilika, jitahidi kuwahi kabla ya muda mliokubaliana. Akifika na kukukuta tayari umeshafika na kumsubiri, ataona umempa kipaumbele, jambo litakalomfurahisha. Mpokee kwa uchangamfu, inuka, muoneshe sehemu ya kukaa na akishakaa na kutulia, na wewe kaa kisha muulize kitu atakachokipendelea.
Anzisha mazungumzo ya kawaida huku ukijitahidi kuwa na tabasamu kwenye uso wako kwani kuna usemi wa wahenga kwamba tabasamu ni kama uchawi wa kimapenzi, hata kama mwenzi wako ana hofu ndani ya moyo wake, akikuona umetabasamu, atatulia na kufurahia kuwa pamoja na wewe.
3. EPUKA MATUMIZI YA SIMU
Watu wengi huwa wanakosea jambo moja, unakuta bibi na bwana wametoka ‘out’ lakini kila mmoja yuko bize na simu yake. Mwanaume yuko bize kuchat Whatsapp au Facebook, mwanamke yuko bize Instagram au kutuma meseji za kawaida.
Nakushauri msomaji wangu usiwe na tabia kama hii kwani haileti picha nzuri. Ikiwezekana, zima kabisa simu yako au itoe mlio ili akili yako yote uielekeze kwa mwenzi wako. Utajisikiaje pale unapomwambia mwenzio kitu kizuri lakini kumbe wala hakusikilizi yuko bize na simu yake? Haileti picha nzuri.
4. EPUKA MATUMIZI YA POMBE KUPITA KIASI
Kama wewe ni mtumiaji wa kilevi, jizuie kunywa hadi kulewa wakati ukiwa kwenye mtoko na mwenzi wako. Kwa kawaida, mtu aliyelewa, hawezi kuzungumza kwa busara, anaweza kufanya jambo lolote la aibu bila kujijua na hawezi kuwa makini katika mazungumzo. Epuka kulewa ukiwa out na mwenzi wako.
5. ZUNGUMZA KWA BUSARA
Badala ya wewe kuwa mzungumzaji mkuu, washauri wa mambo ya mapenzi wanaeleza kwamba ni lazima uongozwe na busara katika kila unachokizungumza. Achana na habari za wapenzi wako waliopita, zungumza naye mambo mazuri ikiwemo mipango ya maisha ya baadaye na jitahidi kuwa msikilizaji kuliko mzungumzaji.
Ni matumaini yangu kwamba ukizingatia haya, utafanikiwa ‘kumroga’ mpenzi wako, ataendelea kukupenda na muda mwingi atakuwa akikufikiria wewe pamoja na kukumbuka mambo mazuri mliyoyafanya pamoja mkiwa out.

Post a Comment

 
Top