
Wabunge wa CCM wamedaiwa kupokea vitisho, kama watakwenda kinyume na msimamo wa chama.
Dodoma. Mpasuko
miongoni mwa wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba wanaotokana na Chama
Cha Mapinduzi (CCM), umechukua sura mpya, baada ya kuelezwa kuwa wabunge
90 wameorodheshwa kwa lengo la kuhojiwa kwa tuhuma za kukisaliti chama.
Wajumbe hao wengi wao wakiwa ni wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano,
wamekuwa wakiitwa na mmoja wa viongozi waandamizi wa Serikali ya CCM na
kuelezwa wazi kuwa chama hakiridhiki na mwenendo wao.
Wengi wa wajumbe hao ni wale waliotamka hadharani kuunga mkono muundo
wa Muungano wa Serikali tatu, badala ya Muungano wa Serikali mbili
ulioboreshwa, ambao ndiyo msimamo wa chama hicho tawala.
Wengine ni wale wanaotajwa kuunga mkono upigaji wa kura wa siri katika
kupitisha vifungu vya rasimu ya Katiba Mpya, ikiwa ni kinyume na msimamo
wa CCM wa kutaka kura ya wazi.
“Ni kweli hata mimi niliitwa na (akimtaja jina) na kuniambia ametumwa
aniletee ujumbe kuwa niko kwenye orodha hiyo na nikiendelea na msimamo
huo nitachukuliwa hatua,” alidai mbunge mmoja.
Hata hivyo, mjumbe huyo alidai kuwa kinachofanywa na CCM ni sawa na
kumpa mgonjwa wa saratani dawa ya kutuliza maumivu, lakini mwishowe
ugonjwa alionao uko palepale.
“Mimi msimamo wangu ambao naamini ndiyo msimamo wa wabunge wengi ni
kutaka kura ya siri na Serikali tatu. Nitasimamia msimamo huo, kwani
ndiyo dhamira yangu kwa masilahi ya Watanzania,” alidai.
Mbunge mwingine anayetajwa kuwapo kwenye orodha hiyo (jina tunalo)
alipoulizwa jana kama ana taarifa hizo alisema, “Ni kweli kuna orodha
hiyo ya wabunge 90, lakini mimi sijaulizwa chochote.”
Mbunge huyo alisema, wabunge hao 90 wamewekwa katika orodha nyeusi
(Black list) iliyoandaliwa na CCM kimeandaa kama njia mojawapo ya
kuwatesa kisaikolojia ili waachane na msimamo wao.
Tayari CCM kupitia kwa Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye
kilishaweka wazi msimamo wake kuhusu suala la muundo wa Serikali na
kutaka wajumbe wake watetee kwa nguvu zote muundo wa Serikali mbili.
Nape: Huu ni uwongo
Nape alipoulizwa jana kuhusu kuwapo kwa orodha hiyo, alikanusha na
kusema huo ni uongo ambao hata shetani ataona aibu kuusema. Chama hakina
mpango wa kuwahoji, alisema na kuongeza;
“Msimamo wa Serikali mbili siyo wa mtu mmoja mmoja, ni msimamo wa CCM na
msimamo wa Watanzania wengi…. Kama kuna haja ya kuwahoji wanaounga
Serikali tatu watahojiwa na wapiga kura wao.”
Ngoma nzito kura ya siri
Wakati CCM wakifanya uamuzi huo, Mwenyekiti wa Muda wa Bunge Maalumu la
Katiba, Pandu Ameir Kificho, ameunda kamati ya maridhiano itakayosaidia
kufikia mwafaka wa kanuni zenye utata na zilizua mabishano makali
bungeni, ikiwamo upigaji kura na Muundo wa Muungano.
Akizungumza bungeni mjini jana, Kificho alisema kamati hiyo imeundwa kwa
ajili ya kutafuta maridhiano katika maeneo ya kanuni ya 32 hadi 43
ambayo yamekuwa na tofauti kubwa.
Alisema makundi mbalimbali katika kamati za vyama vyao na makundi
mbalimbali yanayotokana na uteuzi wa Rais kwenye wajumbe 201, ambapo
kutokana na wingi wao walipewa nafasi ya kukutana katika Ukumbi wa Pius
Msekwa.
Kificho alisema amefikia uamuzi huo ili wiki ijayo waanze kazi ya kupitia na kuichambua rasmi Rasimu ya Katiba.
Hata hivyo, baada ya kauli hiyo, wajumbe kadhaa waliibuka wakiomba
miongozo akiwemo, Dk Ave Maria Semakafu, aliyeshauri uteuzi wa Kamati ya
Maridhiano kuzingatia usawa wa kijinsia katika upande wa kundi la watu
201.
“Ningeomba busara hiyo kuanzia siku tulipojadili iwe inaongoza uteuzi
wote kwa kuhakikisha katika kila kitu ambacho tunakiweka watu tulioko
humu ndani tuweze kuwakilishwa kihalali,” alisema Dk Semakafu.
CREDITS: UDAKUSPECIALLY BLOG
Post a Comment