Yafuatayo ni baadhi ya mambo ambayo yakizingatiwa
huweza kumsaidia mtu kupata marafiki na kuimarisha upendo kwa wale
alionao.
1. Kujenga mawasiliano na hali ya kukutana mara kwa mara
Urafiki huibuka kati ya watu wanaowasiliana na
kuweza kututana mara kwa mara. Utafiti umeonyesha kuwa watu wanaoishi
katika makazi yaliyo karibu karibu wana uwezo wa kujenga urafiki zaidi.
Hususani imebainika kuwa wale wanaoishi katika maghorofa au katika
nyumba zilizo katika makambi kama ya majeshi au nyumba za Shirika la
Nyumba huwa wanaunda urafiki mara nyingi zaidi kuliko wanaokaa katika
makazi yaliyo mbali mbali. Kwa muhtasari, kadri unavyoishi karibu na mtu
mwingine ndivyo kadri
mnavyokuwa na mawasiliano na kuonana mara kwa
mara jambo ambalo hufanya iwe rahisi kwa yeye kutokea kuwa rafiki yako
na pengine hata kuwa rafiki wa kweli. Vile vile watu wanaopata fursa ya
kuwa pamoja kwa muda mrefu katika shughuli kama vile shuleni au
mafunzoni au kazini huweza kujenga urafiki iwapo wahusika wataamua kuwa
marafiki. Watu wengi wamepata marafiki wa kudumu na wake au waume
kutokana na wale waliokutana nao shuleni au kazini. Licha ya kuwa karibu
kutokana na makazi, elimu na kazi, watu hujumuika pia katika shughuli
za kijamii kama vile burudani au maafa ambazo pia hutoa fursa ya kujenga
urafiki. Katika mikutano hii inayokutanisha na watu fulani mara kwa
mara chukua anwani za wale wenye mwalekeo wa kuwa marafiki na hatimaye
anzisha mawasiliano yanayoweza kujenga urafiki.
2. Kuwa mwenye kuthubutu
Kuna watu ambao katika maisha ya kawaida huwa
wanaitwa watu wenye uchakalamu yaani wanapokuwa kwenye kundi la watu ni
lazima watafanya mambo ambayo yatamfanya kila mtu atambue kuwepo kwao.
Kwa upande fulani mwenendo huu huweza kuchukuliwa kama tabia mbaya
lakini kwa upande mwingine ndiyo inayomwezesha mtu kupata marafiki. .
Anza kwa kujitambulisha wewe na kisha muombe akufahamisha yeye ni nani.
Baadaye anzisha maongezi yatakayowafanya mfahamiane na kukutana mara kwa
mara mahali hapo na hatimaye majumbani mwenu.
Kila itakapotokea nafasi ya wewe kuweza kumsaidia mtu yeyote
uliyekutana naye katika namna hii itumie ili uonekane kuwa ni rafiki.
Msaada huo sio lazima uwe wa kitu unaweza kuwa msaada wa ushauri au
mawazo.
3. Kuwa msikivu na mtu anayesogeleka
Kila mtu hupenda kusikilizwa. Mtu huwaona ni
rafiki wale watu wanaomuonyesha wanamfurahia na kumjali. Ili uweze
kupata marafiki huna budi kuwa na uwezo wa kuwafanya watu wote
unaokutana nao na kuongea nao wajihisi unawafurahia na unawajali.
Wataalamu wa saikolojia husema kuwa “Katika miezi miwili unaweza kupata
marafiki wengi kwa kuwaonyesha watu kuwa unawathamini na unawajali
kuliko idadi utakayopata katika miaka miwili kwa kujaribu kuwafanya watu
wakuthani na kukujali wewe”. Wataalamu hao wanasisitiza dhana hii kwa
kusema, “Unawezaje kufanya watu wakupende au wawe na mvuto kwako iwapo
wewe hutawaonyesha kuwa unawathani na kuwajali. Hivi ni vitu ambavyo
huashiria kuwa unawapenda”
4. Kuwa na maongezi ya kusisimua
Pamoja na kuwa msikivu na unayesogeleka bado kuna
sifa nyingine muhimu ambayo inabidi uwenayo ili uwe na mvuto kwa watu
ambao wangeweza kuwa marafiki watarajiwa. Kila unapokuwa na maongezi na
mtu mmoja au kundi la watu hakikisha una jambo la kusisimua
litakalowapendeza na kuwachangamsha. Katika mikusanyiko ya watu hufurahi
sana kama miongoni mwao huwepo mtu anayewaeleza mambo ya kupendeza na
kuwavutia.
5. Fanya watu wakufahamu
Kadri watu wanavyokufahamu na kuelewa tabia na
hisia zako ndivyo kadri unavyojiongezea fursa za kuweza kupata marafiki.
Kama unataka watu wakukubali na kukupenda huna budi kuwapatia nafasi ya
kufahamu jinsi unavyojisikia jinsi unavyofikiri na unavyotenda shughuli
zako. Inabidi ukubali ukweli kuwa watu wanavyojua fikra na hisia zako
kuna wale watakaokukubali na wengine kutokukupenda. Hii ni kanuni ya
maisha ambayo haiwezi kubadilika. Aidha, kumbuka kadri utakavyojitahidi
kuzuia watu wasikuchukie ndivyo kadri utakavyokuwa unazuia watu
wasikupende.
6. Dhibiti hasira zako
Jambo moja lenye utata na ambalo huweza kuathiri
na hata kuharibu mahusiano na urafiki ni hasira. Hata hivyo
wanasaikolojia wamethibitisha kuwa mtu anaweza kumuonyesha rafiki yake
kuwa amechukia na bado wakaendeleza urafiki wao. Wahenga waliwahi kusema
“Muungwana hakasiriki kwa mashavu” Hata kama umekasirika epuka
kuwakaripia marafiki zako watarajiwa au wale marafiki halisi. Katika
mazingira ambayo unalazimika kumkasirikia rafiki yako zungumza naye kwa
upole na utulivu kwa kuwa maneno makali mara nyingi huumiza.
Post a Comment