0
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimezidi kuilaumu iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba kwa kuandika rasimu iliyojaa mawazo ya wajumbe wake waliotaka muundo wa serikali tatu.

Lawama hizo zilitolewa jana na Katibu Mkuu wa chama hicho, Abdulrahman Kinana, katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Mwembeyanga jijini Dar es Salaam.

Mkutano huo uliandaliwa kwa lengo la kumpongeza Rais Jakaya Kikwete, kwa hotuba aliyoitoa bungeni Machi 21, ambapo Kinana alisema tume hiyo iliyokuwa chini ya kada wao Jaji Joseph Warioba, haikueleza ni makundi mangapi yalitaka serikali tatu.

Kinana alisema Tume ya Mabadiliko ya Katiba walisubiri Mwalimu Julius Nyerere afe ndipo waseme serikali tatu, kwani walikuwepo enzi hizo.

“Muungwana angesema nani kasema nini wakati wa kuchukua maoni, tume haijasema katika mabaraza 171 ni mangapi yalitaka serikali tatu, ukiwauliza mara makaratasi yamepotea, hatukumbuki.

“Tusitoane meno na macho kwa ajili ya Katiba, kwani ikishatengenezwa itawekwa kabatini na viongozi wataendelea kula kuku, umaskini upo palepale, ufisadi upo palepale, alichokisema Rais Jakaya Kikwete ni tahadhari tu, yapo maisha baada ya Katiba,” alisema.

Kinana alibainisha kuwa wamepata taarifa kuwa baadhi ya wajumbe wa Bunge Maalumu kutoka upinzani wamedhamiria kuvuruga vikao vya Bunge ili Katiba mpya isipatikane.

Alisema wajumbe hao wanafanya hivyo baada ya kuona hawawezi kuingiza matakwa yao, kwakuwa wingi wa wajumbe wa CCM unawatisha.

Katika hatua nyingine, Kinana alisema kuwa ziara yake ya siku nne jijini Dar es Salaam ya kukagua miradi imeonyesha namna CCM ilivyopiga hatua katika utekelezaji wa ilani.

Alisema kuhusiana na suala la maji alitembelea Ruvu Chini na Juu na kubaini kuwa ifikapo mwaka 2015 asilimia 72 ya wakazi wa Dar es Salaam watapata maji ingawa Wizara ya Maji inakabiliwa na uhaba wa fedha.

Akizungumzia masuala ya umeme, Kinana alisema anayetaka umeme wa bei nafuu ahamie kijijini, kwani gharama za umeme mijini na vijijini ni tofauti.

Kuhusu mji mpya wa Kigamboni, alisema kuwa watalizungumza suala hilo ili kulipatia ufumbuzi.

“Hatujawahi kuona mji mpya unajengwa kwa kuhamisha watu, kama serikali imeamua mbona hawakuuliza wananchi?” alihoji.

Alisema kuwa matatizo ya walimu yataendelea kutatuliwa ikiwemo serikali kuendelea kujenga nyumba za walimu na kuwapunguzia makali ya ugumu wa maisha.

Kawa upande wa tatizo la ajira, aliitaka serikali kutafuta mbinu zisizo za kawaida za kutengeneza ajira nyingi zaidi ili watu wengi waajiriwe, hasa watu wa chini kwa kutengeneza viwanda vingi.

“Watu wanaojiajiri wapewe nafasi, si mgambo kuwasumbua na kuwadai kodi zisizo na msingi, kodi ndogondogo zinasumbua watu na kupoteza muda,” alisema.

Kuhusiana na tatizo la wizi wa dawa hospitalini, Kinana alisema kuwa serikali imepata suluhisho ambapo dawa zote zitaandikwa Serikali ya Tanzania.

Kinana alisema ifike mahali matatizo yanayoikabili nchi yatatuliwe, kwani wao kazi yao ni kuisimamia serikali na kuwajibishana pale panapokosewa.

Naye Mbunge wa Ilala, Idd Zungu, alisema Bunge halikutunga sheria kandamizi kwa bodaboda na wafanyabiashara bali Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini  (Sumatra) ndio waliotunga kanuni kandamizi. 

Post a Comment

 
Top