0

Mjumbe wa Bunge la Katiba, Mchungaji Christopher Mtikila amedai hataweza kuchangia tena katika mjadala wa Katiba kwa kuwa Ofisi ya Bunge imempiga marufuku kutokana na kauli zake.

Hata hivyo, Katibu wa Bunge Maalumu la Katiba, Yahaya Khamis Hamad alisema kuwa taarifa hiyo kwake ni mpya na haamini kuwa jambo hilo lipo.

“Hili kwangu ni jipya na sidhani kuwa linawezekana na lipo,” alisema Hamad.

Awali Mtikila aliliambia gazeti hili kuwa amepewa barua hiyo Jumatano iliyopita, ikiwa ni majibu ya barua yake aliyoandikia ofisi hiyo ya Bunge kutaka ufafanuzi wa kile alichoeleza kuwa amekuwa akinyimwa haki ya kuchangia bungeni.

“Nilianza kuhisi baada ya kuona kuwa nanyimwa kuchangia, nikaandika barua kuomba maelezo kwa nini ninakosa nafasi ya kuchangia bungeni,” alisema Mtikila na kuongeza;

“Lakini juzi nilipokea barua kutoka kwa Katibu wa Bunge ikinikataza kuchangia tena bungeni kutokana na statement (taarifa) zangu za kukosewa kwa mchakato.”

Alisema kuwa alipomuuliza katibu kulikoni akatazwe kuchangia katika Bunge hilo alijibiwa kuwa ni maagizo kutoka kwa mwenyekiti wa Bunge, Samuel Sitta.

Mchungaji Mtikila alisema kutokana na katazo hilo atamwona Sitta ili amfafanulie tatizo lake.

“Hii imeniathiri sana mimi. Bunge hili limepotoka wanachoangalia ni masilahi yao na si ya nchi,” alisema.

Alisema mchakato wote umekosewa kwa kuwaweka wabunge na wawakilishi kuwa sehemu ya Bunge badala ya wananchi kuchagua wajumbe wa Bunge hilo.

“Hakuna nchi yoyote ambayo imefanya hivyo, wanaharibu mabilioni ya fedha ambayo hayataleta Katiba yenye uhalali yoyote,” alisema.

Alisema endapo Sitta atashindwa kutatua jambo hilo anakusudia kuunganisha katika ushahidi wake kwenye kesi inayopinga mchakato wa Katiba.

Post a Comment

 
Top