KIONGOZI wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe amesema anatarajia kuvunja na kuunda upya Baraza la Mawaziri Vivuli, litakaloshirikisha viongozi wengine wa vyama vya upinzani, wanaounda kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA).
Aidha, alisisitiza kasi ya Ukawa katika kuizunguka nchi na kufanya mikutano mbalimbali, kamwe haijapungua.
Alisema
hayo juzi katika viwanja vya Gombani ya Kale mjini Chake Chake kisiwani
Pemba, ambako viongozi wa Ukawa walifanya mkutano wa hadhara, kuelezea
mambo mbalimbali kuhusu mchakato wa Katiba mpya.
Mbowe
alisema umoja huo unatarajia kuwaungunisha watanzania ili wapate Katiba
mpya, inayotokana na maoni na kuzingatia maslahi yao.
Alifahamisha
kuwa umoja huo una dhamira ya kweli na kwamba kuanzia sasa hawatakuwa
tayari kugawanywa kwa misingi udini, ukabila au maeneo.
Mbowe
ambaye ni Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema na Kiongozi wa Kambi ya
Upinzani Bungeni, alisema kwa kipindi kirefu vyama vya upinzani vimekuwa
vikibaguliwa kwa misingi hiyo.
Aliahidi kuwa vitendo hivyo, sasa vimefikia mwisho.
“Sisi
Chadema tumezushiwa propaganda kuwa ni chama cha Kikristo, na wenzetu
wa CUF wakaambiwa kuwa ni chama cha Kiislamu. Sasa tumegundua kuwa lengo
lao ni kutugawa na sasa hatugawiki tena,” alisisitiza Mbowe.
Mwenyekiti
wa Chama cha Wananchi (CUF), Prof. Ibrahim Lipumba alirejea kauli zake
kuhusu matumizi mabaya ya fedha za umma ndani ya serikali.
Alisema kwamba kama vitendo hivyo vitaachwa viendelee, nchi itashindwa kupiga hatua za maendeleo kwa haraka.
Kwa
upande wake, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia ambaye pia ni
Mbunge aliyeteuliwa na Rais Jakaya Kikwete, alisema kitendo cha baadhi
wa viongozi wa serikali, kudai kwamba iwapo muundo wa serikali tatu
utakubaliwa, Zanzibar itakuwa dola ya Kiislamu ni chokochoko, ambazo
hazina ukweli.
Alisema Waislamu na Wakristo wa Zanzibar, wana uhusiano wa muda mrefu na wa kihistoria, ambao hauwezi kutenganishwa.
Alielezea
historia ya kanisa la Minara Miwili la Zanzibar, ambalo ni miongoni mwa
makanisa yenye historia ndefu katika Afrika Mashariki.
Post a Comment