KATIBU wa
Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye,
amesema kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) ni kundi hatari
linaloeneza chuki na kusambaza uongo kwa wananchi.
Amelifananisha
kundi hilo na Boko Haramu na kwamba tofauti yake ni kwamba UKAWA
linatumia silaha ya kusambaza chuki, fitina kwa lengo la kuwagawa
Watanzania wazalendo.
Nape alisema silaha zinazotumiwa na UKAWA ni kali zaidi kuliko za Boko Haramu ambao wanatumia silaha za moto.
Alisema silaha ya kueneza sumu na uongo katika jamii ni mbaya zaidi kuliko silaha za moto.
Nape alitoa kauli hiyo wakati akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika wilayani hapa mkoani Tabora.
Alisema sumu ya
uongo na unafiki inayoenezwa na UKAWA ni hatari kuliko silaha yoyote na
kwamba lengo la kundi hilo ni kuwagawa wananchi wazalendo.
Nape alisema
sumu hiyo walianza kuieneza wakati wakiwa bungeni, ambapo walifikia
hatua ya kumtukana muasisi wa taifa, Mwalimu Julius Nyerere.
"Hawa jamaa
hawana tofauti na Boko Haramu, wanapita kila sehemu kueneza sumu na
chuki kwa wananchi, ninawaombeni wakija muwapuuze,"alisema.
Kwa upande
wake, mbunge wa Jimbo la Sikonge, Said Nkumba, alisema mtaji wa
wapinzani ni kupinga kila kitu kinachofanywa na Serikali ya CCM.
Alisema viongozi wa upinzani wanazunguka kila sehemu kusambaza uongo badala ya kuwapelekea wananchi maendeleo.
"Wapinzani wote
wanaokuja Sikonge kazi yao ni kusema bila kuacha hata mfuko wa saruji
sasa sijui hayo maneno yao yanaleta faida kwa wananchi," alihoji mbunge
huyo.
Aliwataka wananchi kuwapuuza wapinzani wanotumia muda mwingi kupiga porojo bila ya kufanya mambo ya maendeleo kwa wananchi.
Katika hatua
nyingine, msafara wa Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, jana
ulipokelewa na mamia ya wananchi wa wilaya ya Urambo, wakiwemo madiwani
wawili wa Chama cha CUF.
Kinana ambaye amefuatana na Nape waliwasili Urambo na kupokewa na mbunge wa jimbo hilo, Samuel Sitta, na viongozi wengine wa Chama.
Post a Comment