KANISA la Romani Katoliki Tanzania Jimbo Kuu la Morogoro, Jumamosi iliyopita lilifungisha ndoa iliyotafsiriwa na watu kuwa ni ya ajabu kufuatia bi harusi kuwa na matatizo ya wazi ya akili.
Ndoa hiyo ilifungwa katika kanisa lililopo kwenye Kituo cha Kulea Wasiojiweza cha Amani kilichopo Chamwino, mjini hapa na mfungishaji alikuwa mtumishi wa Mungu, Padri Beatus Sewando.
HISTORIA YA BI HARUSI
Habari zilizowazi zinaonesha kuwa, bi harusi huyo amekulia katika kituo hicho ambacho hulea watu wenye matatizo mbalimbali, wakiwemo wenye mtindio wa ubongo kama alivyo bi harusi huyo.
Alipelekwa kwenye kituo hicho akiwa na miaka sita baada ya wazazi wake kujiridhisha kwamba alikuwa mgonjwa wa akili.
KWA NINI NI NDOA YA AJABU?
Kwanza kabisa ni kitendo cha watu kujaa kwenye ndoa hiyo bila kualikwa tukio ambalo lilimshangaza padri huyo mpaka kusema:
“Naona miujiza ya Mungu ikiendelea kutendeka mahali hapa. Sijaalika mtu yeyote lakini nashangaa watu wamealikwa na Mungu na wamejaa hapa kanisani. Pia namuona mpaka mwandishi wa habari (Shekidele) kaja kwenye ndoa hii. Naweza kusema imefana kuliko baadhi ya ndoa nyingine.”
WASIMAMIZI WAPATA KAZI YA ZIADA
Ilikuwa kazi kubwa kwa wasimamizi wa maharusi hao (bestman na matron) kwani iliwalazimu kila wakati kuwaweka chini ya ulinzi maharusi, hasa bi harusi ambaye mara kwa mara alionekana kutaka kutoka na kwenda kusikojulikana.
BI HARUSI AMVISHA PETE BWANA HARUSI KWENYE DOLE GUMBA
Katika hali isiyotarajiwa, ilipofika wakati wa kuvishana pete za ndoa, bi harusi huyo aliipeleka kwenye dole gumba la bwana harusi hali iliyosababisha ndugu kuingilia kati ili pete hiyo iingie kwenye kidole kinachostahili.
Baadhi ya watu waliangukua kicheko kwa tukio hilo wakiona kama burudani ya kipekee ndani ya kanisa hilo.
BI HARUSI AKWEPESHEA USO KUKWEPA BARAKA
Wakati wa maharusi kubarikiwa ulifika ambapo bi harusi huyo alishangaza watu na kuibua kicheko tena baada ya kukwepeshea uso wake upande wenye madhabahu ya kanisa hilo.
MTOTO WA MAHARUSI AVAMIA MBELE
Katika hali nyingine ambayo si ya kawaida kwa siku ya ndoa, ni kitendo cha mtoto mkubwa wa maharusi aitwaye Daudi kuvamia waliko wazazi wao na kukaa nao huku akionesha uso wa kutokuwa na shaka juu ya tendo hilo.
KWA NINI KANISA LILIAMUA HIVYO?
Kwa mujibu wa padri huyo, kanisa lilifikia uamuzi wa kufungisha ndoa hiyo baada ya wawili hao kuishi kwa miaka sita na kuzaa watoto wawili, Daudi (5) na Amos (3).
MAHUBIRI YA PADRI
Akihubiri kabla ya kufungisha ndoa hiyo, Padri Sewando aliwapiga madongo viongozi wa madhehebu na dini nyingine wanaogoma kufungisha ndoa watu wenye ulemavu, hasa wa akili.
“Hebu niambieni kwenye vitabu vyetu vya dini ya Kikristo na Kiislam kuna aya gani inayosema wagonjwa wa akili wasifungishwe ndoa? Hawa ni binadamu wenzetu wana haki sawa na sisi ya kuoa au kuolewa. Mfano, hawa wamekaa katika uchumba sugu zaidi ya miaka sita wanajichunguza na sasa wameamua kuja mbele za Mungu kutubu dhambi zao na kubariki ndoa yao.
“Sasa kiongozi wa dini anapokataa kufungisha ndoa yao maana yake ni nini? Waendelee kuzini? Na hili liwe somo kwa watu wanaoishi katika uchumba sugu kwa muda mrefu.
“Wagonjwa wa akili wameungama na kubariki ndoa yao nyinyi je? Hili liwe somo zuri kwenu,” alisema padri huyo.
Wanandoa hao wakivishana pete.
AMTAJA MTUME MUHAMMAD (S.A.W)Padri huyo aliendelea kusema: “Nawasihi tufuate mafundisho ya Bwana Yesu na Mtume Muhammad (S.A.W) kuwasaidia ndugu zetu wenye matatizo mbalimbali.
“Bwana harusi amefaulu jambo hilo kwani licha ya yeye kuwa na matatizo kidogo ya akili lakini ameamua kumuoa Jamini ambaye muda mfupi ujao atabatizwa na kupewa jina jipya la Maria.
“Mimi ni Mkurugenzi wa Kituo cha Amani, Jamini tumemlea zaidi ya miaka nane sasa, tunamjua ana matatizo ya akili lakini hivyo bwana harusi ameamua kufunga naye ndoa na kubeba msalaba huo wa kumtunza mkewe siku zote za maisha yao. Haya ndiyo mafundisho ya Yesu na Mtume Muhammad.”
BI HARUSI AHOJIWA, AJIBU NDIVYO SIVYO
Baada ya ndoa hiyo, mwandishi wetu alimuuliza bi harusi anasemaje kuhusu tukio hilo la kufunga ndoa, lakini akachanganya mtazamo, msikie:
”Mtujengee nyumba (bila kumtaja nani ajenge), pale tunapokaa baadhi ya wapangaji wenzetu wanatuchokoza.”
BWANA HARUSI AELEZA TABIA YA MKEWE
Naye bwana harusi alipohojiwa kuhusu ndoa yao alisema: ”Nampenda sana mke wangu. Namshukuru kwa kunizalia watoto wawili. Kiukweli kama alivyosema padri kwenye mahubiri yake, mke wangu hana akili hata moja. Ukimtuma sokoni anarudi mikono mitupu, ukimuuliza anasema pesa zimepotea.
“Hawezi kupika, akipika anaweka chumvi nyingi sana au anaunguza chakula. Hivyo mimi kabla ya kwenda kwenye kazi yangu ya kuzibua vyoo na mitaro, nawapikia chakula na watoto nikirudi jioni napika tena.”
Bwana harusi huyo alisema kama kuna mtu ataguswa kumsaidia kumtafutia kazi nyingine au kumsaidia pesa awasiliane naye kwa simu ya Padri Sewando ambayo ni 0754 314 412.
SHERIA ZA NDOA
Kwa mujibu wa sheria za Tanzania katika kujamiiana, ndoa hutenguliwa pale itakapothibitika kuwa mmoja wa wanandoa hao ana matatizo ya akili. Haikuweza kujulikana mara moja kanisa hilo lilitumia kigezo gani kufungisha ndoa hiyo huku mmoja wa maharusi akiwa hajitambui.
>>UWAZI GPL
Post a Comment