0


Mtu mmoja Jabiri Joseph anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka kati ya 25 hadi 30 amekufa baada ya kujinyonga kwa kutumia mkanda wa suruali yake.
 

Kwa mujibu wa polisi, mtu huyo inasadikiwa alijitundika kwenye nondo ya dirisha la chumba cha nyumba alimokuwa akiishi.
 

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, jijini Dar es Salaam Camilius Wambura alisema hayo jana na kuongeza kuwa tukio hilo limetokea juzi jioni katika Kata ya Mabibo.
 

Kamanda Wambura alisema polisi walikuta mwili wa marehemu ukiwa umeketi kitandani  kwake. Hata hivyo alisema kwamba chanzo cha kifo kinaendelea kuchunguzwa na mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.
 

Katika hatua nyingine, polisi waliendesha msako katika maeneo ya Mburahati, Manseze, Mabibo na Kigogo na kuwakamata watuhumiwa 50 wakiwa na kete 155 za bangi, misokoto 50 na pombe haramu ya gongo lita 75.
 
Watuhumiwa hao ni Juma Shinda (36), Tabaya Alex (37), Abdi Juma (25), Sudi Idd(33), Rosemary Mohammed(30), Mariamu Bakari (50) na wenzao 44.
 
Aidha katika tukio jingine, Kamanda wa Polisi mkoa wa Ilala, Marietha Minangi  alisema watu 10 wamekamatwa kwa tuhuma za kukutwa na bangi puri sita pamoja na pombe haramu ya gongo lita nane.
 
Watuhumiwa hao ni Laurent Vicent (40), Lisa Johannes(33), Ali Said(32) na wenzao saba. Watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani baada ya upelelezi kukamilika.

Post a Comment

 
Top