0


Waziri Mkuu Mizengo Pinda anasema ikiwezekana Kanuni za Kudumu za Bunge zirekebishwe ili kuwabana wabunge wa Upinzani wanaotoka bungeni. 
 
Aidha, amewataka wabunge kuheshimu mamlaka ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na kumwachia jukumu la kufanya ukaguzi kuhusu suala la malipo kwa Kampuni ya IPTL. 
 
Waziri Mkuu Pinda aliyasema hayo juzi jioni wakati alipopewa fursa na Spika Anne Makinda kuzungumza muda mfupi baada ya kupitishwa kwa bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka 2014/15. 
 
“Kama inawezekana basi Kanuni zingeweza kurekebishwa, maana jambo hili sio zuri hata kidogo,” alisema Waziri Mkuu na kushangiliwa na wabunge ambao wengi walikuwa ni wa Chama Cha Mapinduzi, na wachache wa upinzani waliobaki. 
 
Wabunge wa Upinzani wakiongozwa na Kiongozi wao, Freeman Mbowe walitoka bungeni juzi jioni, wakisusa bajeti ya Nishati na Madini kwa madai kuwa wabunge wa CCM walikuwa wamejipanga kuipitisha, na hivyo kushiriki kwao ni 'kulinajisi Taifa'. 
 
Waziri Mkuu alisema inamuumiza sana kwa sababu asubuhi wabunge hao wa Upinzani walishiriki kikao, na kutoa maoni yao, tena kwa maneno mengi. 
 
“Kwa kweli mimi kinaniumiza sana, asubuhi walikuwapo, wakatoa maneno yao, halafu jioni watu hawa eti wanatoka nje,” alisema Pinda na kuongeza: 
 
“Hizo ni dalili za kushindwa hoja, wakaona njia rahisi ni kutoka. Mnyika (John) alisema maneno mengi hapa, akapiga blah blah kwa kusoma vichwa vya habari. Sasa baadaye wanatoka. Jibu lake si kutoka. 
 
“Mheshimiwa Spika, tabia hii inazidi kuongezeka, kama inawezekana, basi Kanuni zingerekebishwa, kwa sababu jambo hili sio vizuri hata kidogo.” 
 
Wabunge wa Upinzani wamekuwa na tabia ya kususa vikao vya Bunge mara kwa mara kutokana na madai mbalimbali, hali ambayo sasa imeanza kuzoeleka miongoni mwa Bunge na jamii ya Tanzania. 
 
Kuhusu suala la IPTL, Waziri Mkuu aliwataka wabunge kuheshimu mamlaka ya CAG kwani imeundwa kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania Ibara ya 143. 
“Kwa kweli ofisi hii tunaitegemea sana na isianze kujengeka dalili kuwa pengine hatuna imani na chombo hiki. Hii itatuletea tabu. 
 
“Tumewakabidhi jukumu wenzetu wafanye kazi na kisha watatuletea majibu kama kuna mgogoro ama ubadhirifu au rushwa,” alisema Waziri Mkuu. 
 
Kwa mujibu wa Bunge, Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali (PAC), iliagiza CAG kwa kushirikiana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), kufanya uchunguzi kwenye malipo ya IPTL katika akaunti ya Escrow ya Benki Kuu (BoT). 
 
Hiyo imetokana na kuwapo tuhuma kwamba fedha hizo zimechukuliwa kinyume cha utaratibu, jambo ambalo Serikali imesema hakuna kilichokiukwa. 
 
Waziri Mkuu aliahidi kuwa baada ya uchunguzi, Serikali haitakuwa na kigugumizi katika kuchukua maamuzi kwa wote ambao watakuwa wameonekana kuguswa na suala hilo bila kujali nyadhifa zao. 
 
“Tutachukua hatua stahili baada ya uchunguzi huu, lakini kwa sasa suala hili ni tuhuma tu na isingefaa kuwashutumu watu. Tena wakati tukiambiwa kuwa ushahidi ulioletwa hapa, makaratasi mengine hayana kitu,” alifafanua Waziri Mkuu. 
 
Akihitimisha mjadala wake, Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo alieleza kwa kina kuhusu suala la kampuni hiyo ya kufua umeme tangu lilipoanza mwaka 1998. 
 
Kwa mujibu wake, fedha hizo zinazolalamikiwa hazikuwa mali ya umma na kwamba zilihifadhiwa kwa mujibu wa amri ya Mahakama kusubiri mzozo wa wamiliki wake. 
 
Alisema Serikali imepata fedha zake kwa mujibu wa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT). 
Naye Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola (CCM), alisisitiza kuwa alichonacho mbunge mwenzake, Christopher Sendeka kuwa nyaraka za ushahidi wa sakata la IPTL, ni sawa na makaratasi ya kufungia maandazi, kwani hayana uhalali. 
 
“Nataka kuweka kumbukumbu sahihi na katika Hansard (Taarifa Rasmi za Bunge). Mheshimiwa Sendeka amelalamika kwa mimi kusema kwamba aliyonayo ni makaratasi ya kufungia maandazi. 
 
“Kwa mujibu wa sheria, hati unapaswa kuwa nazo kama wewe ni custodian (Mwangalizi) wake, siyo kuwa na photocopy sijui za IPTL, nyingine za Hong Kong, na Tanesco. Hizi hazina authentic (uhalisia). Atulie. Hizi ni sawa na makaratasi ya kufungia maandazi kule kwenye mgahawa jimboni kwangu. Angesema ana taarifa ningeelewa, lakini siyo ushahidi,” alisema Lugola. 
 
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu Pinda amesema Serikali italiangalia ukweli wa tuhuma zinazomkabili Balozi wa Uingereza nchini, Diana Malrose. 
 
Juzi, Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Stephen Masele akichangia hoja ya bajeti ya wizara hiyo, alimtuhumu Malrose kuingilia masuala ya ndani ya Tanzania kinyume cha Mkataba wa Vienna kuhusu masuala ya kidiplomasia na kumtaka ajipime kama anafaa kuendelea kuiwakilisha nchi yake hapa nchini. 
 
Waziri Mkuu Pinda alisema amelisikia jambo hilo na kwamba Serikali italiangalia kuhusu ukweli wake na kuona kinachohitajika kufanyika.

>>Habari Leo 

Post a Comment

 
Top