0
HUKU ajali za barabarani zikizidi kuongezeka kila siku hasa jijini Dar es Salaam, timu ya uchunguzi ya Operesheni Fichua Maovu (OFM) ya Global Publishers, hivi karibuni lilifanikiwa kuyanasa baadhi ya magari kadhaa yanayokiuka sheria za usalama barabarani.
Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mohamed Mpinga
Magari hayo, ambayo yalikuwa kinara wakati wa uchunguzi huo, yakiwemo yenye namba za usajili zinazoonyesha kuwa ni kutoka idara mbalimbali za serikali, yalikutwa yakiendeshwa kwa kasi maeneo yasiyoruhusiwa, yakitanua kinyume na utaratibu na wakati mwingine yakipita katika makutano ya barabara, licha ya taa nyekundu kuwaka.
Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usafiri nchi Kavu na Majini (Sumatra), Ahmed Kilima.
Katika baadhi ya makutano ya barabara kama vile Tazara, Bamaga na Ubungo, magari hayo, ambayo baadhi yao yanaonekana katika ukurasa wa mwisho wa gazeti hili, yalipita kwa mwendo kasi licha ya kuzuiwa na taa, hali ambayo inaleta uwezekano mkubwa wa ajali.
OMF lilishuhudia gari lenye namba za usajili T 896 BQQ baada ya kuvuka huku taa nyekundu zikiwaka, almanusura  limgonge mtembea kwa mguu aliyekuwa akivuka katika makutano ya barabara ya Bamaga, Mwenge wilayani Kinondoni.
Gari hilo lilitokea Mwenge likiwa katika mwendo wa kasi na halikujali kama taa nyekundu zilikuwa zikiwaka (kuashiria lisipite) na magari mengine yanayotokea Sinza kuelekea Sayansi yalikuwa yanapita.
Uchunguzi umebaini kuwa vitendo hivi vya ukiukwaji wa sheria za usalama barabarani hufanyika zaidi wakati askari wakiwa hawapo maeneo hayo, lakini madereva hao huzingatia sana sheria endapo trafiki wakiwa eneo la tukio.
OFM inaendelea na kampeni ya kuyabaini magari yote yanayokwenda kinyume cha sheria za usalama barabarani na kitayafikisha magari yote kwa Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mohamed Mpinga kwa hatua zaidi.
Aidha kwakuwa magari mengi ya daladala pia yamo, OFM itayafikisha kwa Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usafiri nchi kavu na majini (Sumatra) Ahmed Kilima.
>>>CHANZO: GPL/OFM

Post a Comment

 
Top