0


Shirikisho la soka duniani FIFA, limeliangushia rungu la adhabu shirikisho la soka nchini Nigeria NFF, baada ya viongozi wa serikali ya nchi hiyo kushindwa kutimiza masharti waliyopewa tangu mwishoni mwa juma lililopita.
 
FIFA wameichukulia hatua Nigeria kwa kulifungia kwa muda usiojulikana shirikisho la soka nchini humo, kutokana na viongozi wa Serikali kuingilia mambo ya soka hatua ambayo inapingwa vikali na katiba inayoongoza soka duniani kote.
 
Viongozi wa serikali kupitia wizara ya michezo ya nchi hiyo, walidiriki kuwasimamisha maafisa wa soka kwa kisingizio cha kushindwa kuwajibika ipasavyo mara baada ya kikosi cha Super Eagles, kushindwa kufanya vizuri kwenye fainali za kombe la dunia baada ya kutolewa katika hatua ya 16 bora kwa kufungwa na timu ya taifa ya Ufaransa mabao mawili kwa sifuri huko nchini Brazil.
 
Hata hivyo FIFA bado wametoa muda wa viongozi wa serikali ya nchini Nigeria, kwa kuwaarifu kwamba adhabu ya kufungiwa itaondolewa endapo watawarejesha maafisa waliowasimamisha madarakani.
 
Maamuzi ya kufungiwa kwa Nigeria yataiathiri timu ya taifa ya wanawake ya nchi hiyo chini ya umri wa miaka 20, ambayo kwa sasa inajiandaa na fainali za kombe la dunia ambazo zimepangwa kuanza kutimua vumbi nchini Canada kuanzia August 5-24.g

Post a Comment

 
Top