Katika hali ya kawaida msichana au mwanamke hatazamiwi kuwa na ndevu kwenye kidevu, juu ya mdomo, kifuani, tumboni na mgongoni.
Kwa kawaida mwanamke huwa na vinyweleo vilaini, ambavyo jamii imezoea kuviita ‘malaika’.
Wanaume kwa kawaida huwa na ndevu ambazo
huzitofautisha na vinyweleo kwa rangi nyeusi iliyokolea na huwa vigumu
tofauti na vya wanawake ambavyo huwa vilaini.
Mwanamke anapokuwa na nywele nyingi sehemu hizo
humaanisha kuwapo kwa hitilafu za kijenetiki au dosari za ulinganifu wa
vichocheo vya jinsi mwilini mwake.
Wasichana wengine kutokana na urithi wa vinasaba,
wanaweza kuwa na nywele nyingi sehemu mbalimbali za mwili. Hali hii
kitabibu hujulikana kwa jina la ‘hypertrichosis’.
Mitazamo ya kijamii
Wanawake wanapoota ndevu nyingi hukabiliwa na changamoto za kisaikolojia kutokana na kuwa na mwonekano kama wa wanaume.
Mitazamo na mila nyingi za kijamii katika Bara la
Afrika, bado zinakumbatia unyanyapaa wa wazi au wa kificho kwa wasichana
wanaoota ndevu nyingi.
Msichana mwenye ndevu nyingi, anavuta hisia na
macho ya wanaume na wanawake wenzake pia kiasi kwamba, anatazamwa kwa
namna ambayo wakati mwingine inamnyima raha.
Wapo wanaume wanaoangalia wanawake wa namna hiyo
kwa mtazamo hasi na wengine chanya. Ziko imani potofu miongoni mwa jamii
kuwa wanawake wa namna hiyo wanaashiria kuwa na fedha, wengine
wakiamini huwa wanawapiga waume zao na hata wengine kuamini kuwa hawana
hisia za kike.
Ukweli ni kwamba wanawake wengi wenye ndevu huweza
kuwa na hisia za kike kama wengine na hata kupata watoto licha ya
mwonekano wa nje.
Wakati mwingine wanaume hawapendi kuoa wasichana
au wanawake wenye ndevu nyingi kutokana na mwonekano unaowafanya
wasichana hao kuwa kama wanaume.
Sababu za ndevu
Moja ya sababu za wanawake wengi kuota ndevu ni
dosari za ulinganifu katika mfumo wa vichocheo vya mwili hasa vile
vinavyoamua kutokea kwa mabadiliko ya ukuzi wa kijinsia.
Dosari za ulinganifu wa vichocheo vya kijinsia kwa
wasichana zinaweza kusababishwa na mambo mengi ikiwa ni pamoja na
kuzalishwa kwa wingi kwa vichocheo vya ujinsia kutoka katika mifuko ya
mayai na uvimbe katika mifuko ya mayai.
Uvimbe wa tezi ya Adrenali iliyo juu ya figo pia
unaweza kusababisha tatizo hili kutokana na kuzalisha kwa wingi
kichocheo cha Dehydroepiandrosterone (DHEA).
Wakati mwingine kunakuwepo na hali ya ulinganifu
wa vichocheo vya ujinsia mwilini kama kawaida, lakini tatizo likawa ni
mwitikio wa hali ya juu wa nywele kwa kiasi kidogo na cha kawaida cha
kichocheo cha kiume kilichoko mwilini mwa msichana.
Katika hali hii, msichana pia anaweza kuwa na nywele nyingi sehemu mbalimbali za mwili wake.
Katika utafiti uliowahusisha wanawake 102
wanaokabiliwa na tatizo la kushindwa kutunga mimba waliohudhuria katika
kliniki ya magonjwa ya wanawake, Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH)
kati ya Septemba 2006 na Februari 2007, ilibainika miongoni mwao,
asilimia 32, walikuwa na uvimbe katika mifuko ya mayai.
Asilimia 56.3 ya wanawake wote wenye uvimbe huo,
walikuwa na tatizo la kuwa na nywele nyingi mwilini ikiwa ni pamoja na
kuota ndevu.
Hii ni kwa mujibu wa utafiti wa Dk Pembe AB na
Abeid MS wa Chuo Kikuu cha Sayansi ya Afya na Tiba cha Muhimbili
(Muhas), uliochapishwa katika Jarida la Kisayansi la Tanzania, Journal
of Health Research la Oktoba 2009.
Utafiti ulibaini kuwa mambo mengine yanayochangia
kutokea kwa tatizo hili ni matumizi ya dawa za hospitalini na vipodozi
vyenye viambata vya dawa kama testosterone na steroid.
Ikaonekana kuwa hayo ni matokeo ya matumizi ya muda mrefu ya kutumia vipodozi hivyo kwa muda mrefu bila kupata ushauri wa afya.
Matumizi makubwa na holela ya baadhi ya dawa zenye
kemikali kama vile Danazol, Cyclosporin na nyingine pia yanahusika
kusababisha tatizo hili.
Shirika la Habari la China (Xinhua), limewahi kuripoti taarifa
ya mwanadada mwenye umri wa miaka 16 aliyejulikana kwa jina moja la Nana
kuwa aliota ndevu nyingi baada ya kupewa matibabu ya hospitalini kwa
kupandikizwa mafuta yanayopatikana ndani ya mfupa (uloto).
Mwanadada huyo alipewa matibabu hayo baada ya kupata tatizo la kupungukiwa damu mara kwa mara lijulikanalo kama Aplasticanaemia.
Wataalamu wa sayansi ya afya ya jamii pia wanauhusisha unene wa kupindukia kwa wasichana na kutokea kwa tatizo la kuota ndevu.
Unene wa kupindukia unaweza kusababisha ongezeko kubwa la kichocheo cha kiume kijulikanacho kwa jina la Androgen ndani ya mwili.
Hali hiyo hutokana na nyama zenye mafuta mengi kugeuza kichocheo cha kike cha estrogen kuwa kichocheo cha kiume cha androgen.
Androgen inapokuwa nyingi mwilini husababisha
msichana kuwa na tabia za kiume ikiwa ni pamoja na kuota ndevu na kuwa
na sauti nzito.
Daktari Adam Nyalandu kutoka Hospitali ya Taifa
Muhimbili (MNH), amewahi kunukuliwa kwenye gazeti moja la hapa nchini
akisema kuwa tatizo la wanawake kuota ndevu linaweza kutokana na sababu
nyingi ikiwamo matumizi ya vyakula vya kusindika vinavyotengenezwa kwa
kutumia kemikali nyingi.
“Mfano ulikuwa huli nyama za kopo au vyakula vya
kusindika ambavyo kemikali inatumika kuvisindika sasa unakula, vinaweza
kusababisha tatizo hilo kwa kiwango kikubwa,” anasema Dk Nyalandu.
Wanawake wenye ndevu mara nyingi hukabiliwa na
dalili kadhaa zinazowafanya watafute msaada wa kitabibu mara kwa mara.
Baadhi ya dalili hizo ni kama vile kuota chunusi nyingi, kutokupata
hedhi kama kawaida. Wakati mwingine msichana hupata damu pungufu wakati
wa hedhi au kutoiona kabisa. Wataalamu wanasema wakati mwingine wanawake
wa namna hiyo hupata hedhi isiyo na mpangilio.
Wanawake wenye tatizo hili pia wanakabiliwa na uwezekano wa kupata magonjwa sugu ya muda mrefu.
“Kama utafanya mahesabu, utagundua kwamba angalau
nusu ya wanawake wenye tatizo la kuwa na nywele nyingi mwilini,
wanakabiliwa na hatari kubwa ya kupata magonjwa ya kisukari na moyo,”
anasema.
Daktari bingwa wa magonjwa ya mfumo wa vichocheo
vinavyohusiana na mfumo wa uzazi mwilini na Rais wa Chuo Kikuu cha
Sayansi za Afya cha Georgia, Dk Ricardo Azziz akielezea umuhimu wa
utafiti alioufanya kwa kushirikiana na Vituo vya Afya vya Heather Cook
na Kathleen Brennan, anasema matatizo mengine yanayosababisha ndevu
kuota kwa wingi pia yanaweza kumfanya mwanamke kuwa mgumba.
Hali hiyo pia huweza kuandamana na kusinyaa kwa matiti na mfuko
wa mji wa mimba. Athari nyingine ni pamoja na kututumuka isivyo kawaida
kwa maumbile ya via vya uzazi na kuwa na sauti nzito na wakati mwingine
kisanduku cha sauti hunenepa kama cha wanaume.
Mtawanyiko wa nywele mwilini huwa kama wa kiume.
Pamoja na ndevu msichana huota nywele kifuani, tumboni, mapajani,
mgongoni, miguuni na mikononi kwa wingi.
Epuka athari kisaikolojia
Ili kuepuka athari za kisaikolojia zinazoweza
kutokana na hali hii, msichana anashauriwa kuelewa kuwa kuota ndevu siyo
dhambi na wala kosa.
Anapaswa kufahamu kwamba ndevu hazipaswi kuwa
chanzo cha msongo wa mawazo kwani hali hiyo inaweza kuathiri afya ya
mwili na akili.
Pia, ndevu zisiachwe zikawa ndefu kama za wanaume
kwani zinavuta hisia za watu kumwangalia mwanamke au msichana kiasi
kwamba hali hiyo inaweza kusababisha matatizo ya kisaikolojia.
Ndevu zikatwe na kuwa fupi kadri inavyowezekana
wakati wote. Mkasi au cream ya kuondoa nywele inaweza kutumika kwa lengo
hili. Ile dhana ya wanawake wengi kwamba ndevu zikinyolewa zinaongezeka
maradufu haina ukweli wowote wa kisayansi.
Ndevu zising’olewe kwa vidole. Hii inaweza
kusababisha uambukizo wa bakteria katika ngozi kwa urahisi na kuleta
matatizo makubwa ya kiafya.
Njia nyingine iliyo bora kwa wasichana kujiepusha
na tatizo la kuota ndevu ni kuachana na matumizi ya vipodozi vyenye
viambata vya steroidi vinavyoleta weupe bandia wa ngozi.
Kufanya mazoezi ya mwili na kudhibiti unene wa
mwili kwa njia ya lishe bora pia ni mkakati mwingine unaosaidia
kupambana na tatizo hili.
Endapo nywele zimetapakaa kwa wingi miguuni na
mikononi na kuleta mwonekano wa kiume, ni bora kuvaa nguo ndefu
zinazofunika mwili vizuri ili kuepuka msongo wa kisaikolojia ambao
unaweza kutokea kutokana na mtazamo hasi wa kijamii.