0
Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo ya Mengwe, Adinani Kingazi amemhukumu kifungo cha miaka mitatu jela, Gedfrey Kimaria (35) baada ya kukutwa na hatia ya kumjeruhi vibaya mtoto wa miaka sita kwa kumng’ata mgongoni kwa madai ya kuiba paka.
 
Kesi hiyo ilivuta hisia za watu wilayani Rombo mkoani Kilimanjaro na wananchi wilayani humu walifurika katika mahakama hiyo kusikiliza hukumu ya kesi hiyo.
 
Akitoa hukumu hiyo, Hakimu Kingazi alisema mnamo tarehe 29 Septemba mwaka huu saa kumi na mbili na nusu jioni katika Kijiji cha Mamsera juu mshtakiwa alifanya kosa hilo kinyume na kifungu cha 241 cha sheria ya makosa ya jinai sura ya 16 cha kanuni ya adhabu.
 
Hakimu huyo alisema mshtakiwa alifanya ukatili huo kwa mtoto Dilex Lyakurwa (09).
 
Hakimu Kingazi alisema mshtakiwa alimshambulia mtoto huyo kwa kile alichodai kuwa mtoto alienda kuchota maji nyumbani kwake na wakati akirudi kwenda nyumbani paka wa mshtakiwa alimfuata mtoto huyo na baadaye paka huyo aligoma kurudi ndipo mshtakiwa alikasirika na kumshambulia kwa madai kuwa amemwibia paka wake.
 
Hakimu alisema mahakama hiyo imeridhishwa na ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka pamoja na vielelezo vya polisi vilivyoletwa mahakamani ikiwamo taarifa ya daktari ambayo inaonyesha mtoto huyo aliumizwa.
 
Alisema katika taarifa ya daktari iliyowasilishwa mahakamani hapo, ilionyesha kuwa mtoto huyo alichomwa na kitu chenye ncha kali mgongoni.
 
Alisema mshtakiwa atatumikia kifungo cha miaka mitatu jela na baada ya kumaliza adhabu atamlipa mlalamikaji Sh200,000 kama gharama za matibabu pamoja na fidia ya maumivu aliyoyapata.

Post a Comment

 
Top