0
WALIOMO wamo, wasiyokuwemo nao wameingia! Ni msemo ulioanza kusikika tangu Jumanne iliyopita kufuatia makabrasha ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) iliyo chini ya Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe kuvuja na kuonesha ikimtaja Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kama kiongozi anayeingia kwenye kashfa ya mabilioni ya Escrow.

Pinda au ‘Mtoto wa Mkulima’ ambaye jana alijieleza kwenye bunge, kamati ya Zitto ilisema aliujua mchezo mzima wa kuchotwa kwa shilingi bilioni 306 kutoka Akaunti ya Tegeta Escrow kwenda Kampuni ya IPTL.
Kamati ya Zitto ilimtaja Pinda kwa cheo chake cha uwaziri mkuu kwamba alitakiwa kuhakiki kama si kuthibitisha kwamba, malipo ya mabilioni hayo kwenda IPTL yalikuwa sahihi au la jambo ambalo kamati ilidai hakulifanya.
Baadhi ya wananchi waliozungumza na Ijumaa jana walisema kilichomponza Mtoto wa Mkulima ni kupelekewa makaratasi mezani yenye mapendekezo ya mabilioni hayo kulipwa IPTL kisha yeye kumwaga wino bila kuthibitisha kwa mapana uhalali wa kwenye makaratasi hayo.
“Unajua Pinda kaingia kikaangoni kwa sababu ya kutoku-verify (kuthibitisha). Yeye aliwaamini sana akina Maswi (Eliakim, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini) akijua wanachompelekea ndiyo sahihi,” alisema Jumanne Bakari, mkazi wa Kinondoni jijini Dar.
Naye, Silisia Magushi, mkazi wa Kigamboni, Dar yeye alisema: “Pinda ameponzwa na kauli zake. Aliposema bungeni kwamba fedha za Escrow si za umma bali za IPTL pale ndipo kwenye tatizo la msingi. Tena alisema kwa uhakika na kujiamini sana.
“Yeye kama waziri mkuu ina maana alikuwa hajui kama fedha zile ni za umma? Mbona Gavana wa Benki Kuu, Beno Ndulu alijua, mbona Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru (Edward Hosea) alijua, iweje yeye waziri mkuu wa nchi asijue bwana?!”
Wasomaji wengi wa Ijumaa walisema Pinda amejikuta kwenye matatizo kwa sababu ya kauli zake na kutosimamia vyema ulinzi wa fedha hizo za umma kwa vile kwenye mgawo wa fedha hakutajwa kama alivyotajwa Anna Kajumulo Tibaijuka na Andrew John Chenge, labda kama alipewa kwa ‘mkono wa nyuma.’
Jana, sakata la kuchotwa kwa Fedha za Akaunti ya  Tegeta Escrow lilishika kasi bungeni mjini Dodoma ambapo watuhumiwa viongozi walipewa nafasi ya kujieleza akianza Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo na baadaye mjadala ukaanza.
Kashfa hiyo iliibuliwa kwa mara ya
kwanza na Mbunge wa Kigoma Kusini
(NCCR-Mageuzi), David Kafulila katika kikao cha Bunge lililopita madai ambayo yalipingwa kwa nguvu kubwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema na Waziri wa Nishati na Madini, Sospeter Muhongo.

Ukiacha Anna Tibaijuka ambaye ni Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, mwanasheria mkuu wa zamani wa serikali, Chenge naye ametajwa kuchotewa kiasi cha shilingi bilioni 1.6.
Akaunti ya Tegeta Escrow ilifunguliwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ili kutunza fedha ambazo Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (Tanesco) zilipaswa kuilipa kampuni ya kufua umeme ya IPTL kwa kuiuzia nishati hiyo.
Hiyo ilitokana na shirika hilo la umma, kushtaki katika mahakama ya kibiashara ikilalamikia bei kubwa iliyotozwa na IPTL na kusababisha kufunguliwa kwa akaunti hiyo ili fedha hizo ziwekwe huko hadi muafaka baina ya pande hizo mbili utakapopatikana.

Hata hivyo, kabla ya muafaka huo kupatikana, wajanja walikwenda na kuzichukua fedha hizo ambazo zimewatokea puani!
Chanzo: GPL

Post a Comment

 
Top