Kuna dhana imejengeka sana huku mitaani kuhusu uhusiano au ndoa na mtoto. Watu wanaamini kuwa watoto wana nafasi kubwa ya kuongeza upendo katika maisha ya wenza wawili. Kwamba ndoa isiyo na mtoto haiwezi kuwa imara na yenye upendo.
Wanawake wamekuwa na imani kuwa kama hawana watoto katika ndoa zao, basi mapenzi kutoka kwa waume au marafiki zao yanakuwa na mashaka ya kuweza kustawi. Ni kutokana na sababu hii, wengi wamekuwa wakikimbilia kwa waganga wa kienyeji wakiamini huko wanaweza kupewa mitishamba itakayowawezesha kupata watoto wa kuimarisha ndoa zao.
Hili la waganga wa kienyeji litakuwa na siku yake rasmi ya kulizungumzia, lakini leo ningependa kujikita kwenye swali hili la msingi, kama ni kweli kwamba kuzaa mtoto katika ndoa au uhusiano kunaongeza au kudumisha uhusiano wako.
Kibinadamu, mtoto ni zao ambalo kila mtu katika uhusiano angependa liwepo, kwa sababu hata Mwenyezi Mungu alisema tuje kuijaza dunia. Familia nyingi zinaishi kwa furaha zinapokuwa na watoto, kwani zinakuwa na uhakika wa kuendelea kuwepo kizazi hadi kizazi!
Wapo wanawake wanaoishi kinyonge katika mahusiano mengi wakiwa hawana amani kwa sababu ya kukosa mtoto. Wapo wengine wameshaachika kwa sababu hiyo na wengi wengine wameendelea kutoa machozi kila kukicha kwa vile tu Mwenyezi Mungu hakuwajaalia kupata mtoto.
Tunapozungumzia tafsiri halisi ya mapenzi baina ya wawili wapendanao, suala la kupata au kutokupata mtoto haliwezi kuwa kigezo cha kupendana kwao, vinginevyo labda waingie mkataba, kitu ambacho kimsingi siyo mapenzi.
Mapenzi ni ile hali ya wawili kuishi ndani ya moyo mmoja, kwamba bila uwepo wa mmoja wao, mwingine anakuwa katika wakati mgumu. Kila mmoja anajihisi hajakamilika pasipo mwenzake, na hamu ya kuwa pamoja inabaki kuwa ileile jana, leo kesho na siku zote.
Wapo watu ninaowafahamu walioishi miaka zaidi ya 15 pasipo kupata mtoto, lakini ukiwaona utafikiri wameanza kuishi jana, yaani penzi baina yao halijifichi na mtoto hajawahi kuwa tatizo, ingawa mwanamke ni mtu anayejisikia vibaya mno kwa kukosa mtoto.
Amani au uimara wa ndoa hauletwi na watoto, isipokuwa na namna jinsi wawili walivyoamua kuishi. Zipo familia zilizo na watoto lakini maisha yao ni ya kukatisha tamaa sana, kwa sababu kila siku ni ugomvi, misuguano na presha tupu.
Mtu hawezi kuachana na mwenza wake kwa sababu ya mtoto, kwa vile kwanza licha ya jambo hilo kuwa ni kudra za Mwenyezi Mungu, pia ni kitu kinachozungumzika.
Watu wengi hudhani familia kukosa mtoto ni tatizo la mama pekee, hawajui kuwa wapo hata wanaume ambao wana matatizo ya kushindwa kusababisha ujauzito. Sasa katika uhusiano wa waliopendana kwa dhati, watakaa na kujiuliza, nini chanzo?
Kimsingi, wanaweza kwenda kupata ushauri wa kitabibu kwa mabingwa wa magonjwa ya uzazi. Kama mmoja wao ataonekana kuwa na tatizo, ni wazi kuwa daktari atazungumza kama linatibika au la.
Lakini kama itathibitika kuwa ni tatizo ambalo haliwezi kutibika, bado uwanja ni mpana kwa wapendanao kuamua, ama kukubaliana na hali hiyo maisha yao yote, au kujitoa muhanga na kumruhusu mwenza mmoja ‘kuchepuka’ ili mradi tu kukidhi haja ya mtoto!
Kitu nilichogundua mimi, mwanamke anapokosa mtoto, kutokana na kutojiamini, kila tatizo dogo linapotokea ndani ya nyumba, hukimbilia kutoa madai ya kwamba hayo yote yanatokea kwa sababu ya kukosa kwake mtoto!Nisisitize tu kuwa furaha katika ndoa au uhusiano wako iko ndani ya mikono yako mwenyewe, mtoto ni kisingizio!
Post a Comment