0

AMEKULA chumvi nyingi! Wakati ‘majanki’ wa umri kati ya miaka 20 hadi 40 wakipukutika, kikongwe mwenye umri wa miaka 110, mkazi wa Kiluvya wilayani Kisarawe, Pwani, Ally Said Makongwa amewastaajabisha wengi kufuatia kazi nzito anazofanya ambazo haziendani na umri wake.


Kikongwe kinachosadikika kuwa na  miaka 110 Ally Said Makongwa
Mzee huyo amekuwa akijishughulisha na kazi nzito bila kuhitaji msaada wa aina yoyote kwa ndugu zake hata pale wanapotaka kumsaidia hivyo kuonekana wa ajabu.
Akizungumza na wanahabari wetu, mjukuu wa mzee Makongwa, Ally Makongwa (46) ambaye muda wote amekuwa akihangaika na malezi ya babu yake alisema, babu yake amekuwa akiwastaajabisha kutokana na kitendo chake cha kung’ang’ania kwenda mbali kulima na kukata miti kisha kuchoma mkaa.
“Kusema kweli umri wa babu yangu umekwenda. Ana miaka 110 lakini anang’ang’ania kufanya shughuli ngumu bila kuhitaji msaada. Tukimkataza huwa anasema hawezi kukaa bila kufanya kazi wakati kazi zenyewe anazifanya kwa tabu akiwa amekaa,” alisema mjukuu huyo na kuongeza:
“Isitoshe hata akiumwa huwa hataki kutumia dawa za hospitali na hajawahi kufanya hivyo. Huwa anatumia mti ambao anauamini yeye ni dawa na kutumia dawa asili, yaani vitu vinavyokatazwa yeye ndiyo anavitaka lakini cha ajabu huwa vinamsaidia.”
Pia mjukuu huyo alithibitisha babu yake kuwa na zaidi ya umri wa miaka 110 huku akiweka wazi kuwa alikuwepo hata kabla ya vita ya kwanza ya dunia kati ya mwaka 1914 hadi 1918
Kwa upande wake kikongwe huyo ambaye alikuwa akizungumza na kusikia kwa tabu alisema kuwa katika maisha yake amepitia mambo mengi tangu enzi za utawala wa kikoloni wa Mjerumani na Muingereza na anaendelea kuishi hadi sasa akiwa mwenye nguvu.
Alisema ameweza kudumu kwa kuutumikisha mwili wake bila kubweteka na kula vyakula vya asili.
“Huwa natumia dawa za asili na mboga za majani kwa wingi, vitu ambavyo watu wengi wanavipuuza kwa sasa, ndiyo maana nimefikisha umri huu, si rahisi,
pia nafanya kazi kwa kuwa nina uwezo wa kuzifanya, siwezi kumuaamini mtu kunifanyia kazi zangu, ataniharibia vile ninavyotaka,” alisema mzee huyo kwa tabu huku akiweka wazi kuwa mtoto wake wa kwanza ana umri wa miaka 86 huku mkewe akiwa ameaga dunia baada ya kuishi miaka 90.

Post a Comment

 
Top