0
Tunaishi kwenye ulimwengu wa shughuli nyingi na kazi huku kila mtu au kila familia ikijaribu kwa hali na mali kuhakikisha kwamba mahitaji ya msingi yanapatikana. Hivyo familia nyingi sasa wanajikuta Baba na Mama wote wanafanya kazi huku tukiiacha nyumbani na watu wengine mchana kutwa.
black_child_watching_television-16x9
Swali letu la msingi sasa je ni nani analea na kuchangia tabia za watoto wetu? Kama mzazi unapata muda wa kulea na kufundisha watoto wako utakuwa na bahati na endelea na moyo huo huo. Kwa wale ambao hawajapata muda au hawana muda hivyo hupata muda wakati mwingi ni Jumamosi na Jumapili huku wakidhani wanaweza kubadilisha kilichowekwa kwa watoto wao kutoka Jumatatu hadi Ijumaa, unahitaji muujiza tu. Hebu tuangalie, kitu gani kinaendelea kwenye nyumba zetu;
Jamii ina wazazi wengi lakini haina walezi wa watoto hao. Unaweza ukashangaa ni nini hiki kinaendelea, wakati wewe unakuwa ilikuwa ni rahisi kwa mama yako kujua tabia yako hatua kwa hatua. Lakini sasa inakuwa ngumu kwani unafanya kazi na hauna muda wa kujua mtoto au watoto wako siku nzima wameongea na nani, wamekutana na nini na wamejifunza nini kibaya na unamfundishaje kuwa hicho ni kibaya? Kazi zetu zinatuhitaji sana kiasi kwamba tumetoa sadaka familia zetu kwa ajili ya mshahara wa kila mwezi huku tukiacha watoto hawana sehemu ya kujifunza au wanajifunza kwa watu ambao si sahihi kwaajili ya maisha ya baadaye.
Wazazi wamewaachia watu wasio na vigezo ndio walee watoto wao. Inawezekana wewe ni mtu mkubwa na mwenye cheo kizuri au kazi nzuri, ulipokuwa unaajiriwa uliulizwa vyeti na uzoefu wa kazi na mara nyingine hata chuo ulichosoma ni kigezo cha kutosha. Umepata kazi na wewe inabidi utafute mfanyakazi wa kulea watoto wako unapokuwa kazini, je umetumia vigezo gani kumpata mfanyakazi huyo?
Wewe una elimu ya kukutosha kufanya kazi kwa mwajiri wako lakini anayetunza familia yako hana vigezo akijitahidi sana ni darasa la saba, hivyo usitegemee matokeo zaidi ya darasa la saba. Watoto wako watajifunza tabia za huyo dada wa kazi na sio tabia zenu kama wazazi na watarithi kutoka kwao kuliko kwenu hata upendo wao watachukua kwao na sio kwenu. Utagundua pamoja na elimu uliyonayo na namna unavyoheshimika, nyumba yako inaongozwa na kiongozi ambaye hana vigezo wa darasa la saba au chini ya hapo, je tunajenga au tunabomoa?
Wewe kama mzazi una malengo gani na kizazi chako hapo baadaye? Kumbuka sio wewe unaelea hicho kizazi, yaani wewe ni mashine ya kuzalisha tu, bali anayekuza na kutengeneza tabia na mwenendo ni mtu mwingine kabisa ambaye hata sio wa ukoo wako na hana elimu ya kutosha kukuza familia yako na bado hujashituka kwanini watoto wanatabia hizo walizo nazo na wamepata wapi? Imeandikwa apandacho mtu ndicho atakachovuna, unastahili kuvuna ulichopanda kwa watoto wako, kama hujapanda tabia njema usitegemee kitu kizuri kutoka kwao na kwa upande wa pili ni sahihi kabisa. Kazi kwako ni nani analea na kuchangia kukuza tabia za watoto wako?
Tunahitaji kufanya maamuzi magumu lasivyo kizazi kitapotea kwa kukosa malezi ya baba na mama. Ni kweli tunahitaji pesa na vitu vingi vizuri, pia tunahitaji busara ya kutosha kujua namna ambavyo tunajipanga kulea kizazi hiki. Bila hivyo kizazi hiki kitalelewa na katuni za DSTV au Startimes kwa ushirikiano na dada wa kazi kama mama na shamba boy au mlinzi kama baba. Kazi kwako, huu ni mtizamo tu, majibu unayo mwenyewe na kuchukua hatua ni jukumu lako binafsi.

Post a Comment

 
Top